IQNA

Msikiti mpya wafunguliwa Uholanzi

12:36 - June 23, 2019
Habari ID: 3472012
TEHRAN (IQNA) – Msikiti mpya uliopewa jina la Masjid Tawheed umefunguliwa mapema wiki hii katika mji wa Venlo, kusini mashariki mwa Uholanzi.

Kwa mujibu wa taarifa, msikiti huo umejengwa kwa ufadhili wa Idara ya Masuala ya Kidini Uturuki inayojulikana kama Dianat.

Ujenzi wa msikiti huo ulisimamiwa na Taasisi ya Wakfu ya Uholanzi mwaka 2016 na umefunguliwa rasmi Juni 21 baada ya Sala ya Ijumaa. Msikiti huo uliojengwa kwa usanifu majengo wa Kiislamu una nafasi ya waumini 2500. 

Akizungumza wakati wa ufunguzi wa msikiti huo, Ali Arbash, Mkuu wa Idara ya Dianat ya Uturuki amesisitiza umuhimu wa nafasi ya misikiti barani Ulaya na kusema ujenzi wa misikiti na vituo vya kidini ni moja ya mbinu muhimu zaidi ya kuimarisha umoja na mshikamano wa Waislamu.

Akizungumza katika hafla hiyo, Balozi wa Uturuki nchini Uholanzi Sha'ban Dishli amesema lengo la ujenzi wa msikiti huo ni kuwapa fursa raia wa nchi hiyo kuufahamu Uislamu.

Naye Imamu wa msikiti huo Sheikh Ahmad Dursun amesema Msikiti wa Tawheed unalenga kuarifisha mafundisho ya Kiislamu na kueneza amani na udugu katika jamii.

Pembeni mwa sikiti huo kuna ukumbi wa mikutano, kituo cha kutoa mafunzo ya Kiislamu mgahawa na eneo la kuegeshea magari.

3821279

captcha