IQNA

Watawala Saudia wamkamata mwanazuoni anayepinga ufasiki, ufisadi

19:05 - September 11, 2019
Habari ID: 3472126
TEHRAN (IQNA) – Mwanazuoni wa kidini nchini Saudi Arabia amekamatwa baada ya kukosoa sera za ufalme za kuwakaribisha watumbuizaji wa kimataifa wanaoeneza ufasiki na ufisadi wa kimaadili.

Kwa mujibu wa taarifa,  maafisa wa usalama wamemkamata Sheikh Omar al Muqbil ambaye amenukuliwa akikosoa Mamlaka ya Burudani na Starehe ya Saudi Arabia kwa kuvuruga maadili na utamaduni wa nchi kwa kuwaalika wasanii na watumbuizaji wa Kimagharibi nchini humo.

Sheikh al Muqbil ametoa matamshi hayo katika hali ambayo mrithi wa Ufalme wa Saudi Arabia Mohammed bin Salman al maaruf MBS amekuwa akiongoza kampeni ya uliberali wa kijamii, ambayo kati ya mengine inahimiza wanamuziki na wasanii wa Kimagharibi wenye kueneza ufasiki na ufisadi wa kimaadili  kualikwa Saudia kwa lengo la kuwatumbuiza wananchi.

Kampeni hiyo ya MBS  ya kueneza utamaduni mbovu wa Kimagharibi imeandamana na oparesheni maalumu ya kuwakamata wale wote wanaompinga hasa wanazuoni wa kidini.

Hadi sasa wanazuoni na wasomi waliokamatwa Saudia ni pamoja na Abdul Aziz al Fawzan, Imamu wa zamani wa Msikiti wa Makka, Sheikh Saleh al Taleb,  Sheikh Safar al Hawali na mwanazuoni maarufu Sheikh Salman al Odah.

Kesi ya al Odah ni tafauti kwani yeye yuko gerezani kwa kutoa wito wa kuwepo maelewano baina ya Saudi Arabia na Qatar baada ya nchi hizo mbili jirani kukata uhusiano mwaka 2017. Hivi sasa al Odah anakabiliwa na hukumu ya kunyongwa. Wanazuoni wengine wa Saudia ambao wamepangwa kunyongwa kwa tuhuma bandia za ugaidi ni pamoja na   Sheikh Awad al-Qarni na Ali al-Omari.

Kampeni ya utawala wa Saudia dhidi ya wapinzani haishii ndani ya mipaka ya nchi hiyo kwani Oktoba mwaka 2018, maafisa wa usalama wa Saudia walimuua kinyama mpinzan mkubwa wa Bin Salman, Jama Khashoggi ndani ya ubalozi mdogo wa Saudia mjini Istanbul, Uturuki.

Ikumbukwe kuwa, mapema mwezi Julai mwaka huu, wanazuoni. wanaharakati wa mitandao ya kijamii na wananchi wa Saudi Arabia wamekasirishwa mno na kualikwa mwanamuziki mmoja wa rap wa Kimarekani katika tamasha la muziki la mjini Jeddah.

Taasisi ya Burudani na Starehe ya Saudi Arabia ilikuwa imemualikak mwanamuziki wa Kimarekani, Nicky Minaj kutumbuiza katika tamasha hilo. Hatimaya kufuatia malalamiko makubwa, mamlaka hiyo ililazimika kubatilisha uamuzi wa kumualika Saudia mwanamuziki huyo wa Marekani ambaye ni maarufuku kwa ufasiki wake.

Watawala wa Saudia, ambao wanajinadi kuwa eti ni wahudumu wa Haram Mbili Takatifu za Kiislamu, wako mbioni kuleta mabadiliko yake ya kijamii yanayoiga vigezo vya madola ya Magharibi visivyo vya Kiislamu na visivyo vya kimaadili, jambo ambalo linalalamikiwa vikali na Waislamu Saudia na kote duniani.

/3469381

captcha