IQNA

Wachezaji wa timu ya Newcastle ya Uingereza wapata chumba cha kusalia

17:40 - April 06, 2013
Habari ID: 2515141
Timu ya soka ya Newcastle United ya Uingereza inayoshiriki ligi ya Premia nchini humo imewaandalia chumba maalumu cha kusalia wachezaji wake Waislamu katika uwanja wa mpira wa timu hiyo.
Magazeti ya Uingereza yameandika habari hiyo na kubainisha kwamba, timu ya Newcastle ina wachezaji saba Waislamu na kabla ya kuandaliwa chumba hicho maalumu cha kusalia, wachezaji hao Waislamu walikuwa wakitekeleza ibada yao ya Sala katika vyumba tofauti kabla au baada ya mechi katika uwanja maalumu wa mpira wa timu hiyo wa St James Park.
Wachezaji Waislamu wa timu ya Newcastle ya Uingereza ni Massadio Haidara, Hatem Ben Arfa, Moussa Sissoko, Mapou Yanga-Mbiwa, Cheick Tiote, Papiss Cisse na Mehdi Abeid.
Gazeti la Daily Mirror la Uingereza linaripoti kwamba, mchezaji Demba Ba ambaye hivi karibuni alijiunga na timu ya Chelsea ndiye aliyekuwa akiwasalisha wachezaji Waislamu wa timu yake hiyo ya zamani. Demba Ba anasifika kuwa ni mcha Mungu na mtekelezaji mzuri wa ibada. Siku zote akifunga goli husujudu na kumshukuru Mwenyezi Mungu. Ba anasema, anapenda kusali Sala tano na katu hapendi starehe za pombe na sigara. Wachezaji Waislamu wa timu ya soka ya Newcastle ya Uingereza mbali na kutekeleza ipasavyo ibada ya Sala Tano kwa siku, wana kawaida ya kusali kwa ajili ya kuomba dua kabla ya mechi wakiiombea ushindi timu yao na wengi wao wanapofunga goli husujudu na kumshukuru Mwenyezi Mungu ada ambayo bila shaka inapaswa kuigwa na wachezaji wengine Waislamu.
Timu ya soka ya Newcastle ndio yenye wachezaji wengi zaidi Waislamu kati ya timu zinazoshiriki ligi kuu ya soka nchini Uingereza. 1208341
captcha