IQNA

Uturuki yatuhumiwa kueneza magaidi Ulaya, kuhimiza misimamo mikali

17:18 - March 28, 2016
Habari ID: 3470219
Mfalme Abdullah II wa Jordan ameituhumi Uturuki kuwa inahimiza misimamo mikali eneo la Mashariki ya Kati sambamba na kueneza magaidi bara Ulaya.

Nakala ya siri iliyovuja imefichua kuwa, Mfalme Abdullah wa Jordan aliyasema hayo wakati alipokutana na kufanya mazungumzo na maafisa wa ngazi za juu wa Marekani Januari 11 mwaka huu.

Tovuti ya Middle East Eye imemnukuu mfalme huyo ambaye alisema kuwa: "Misimamo mikali inazaliwa Uturuki na kwamba nchi hiyo imekuwa ikituma makundi ya watu wenye misimamo ya kufurutu ada kwenda bara Ulaya.”

Mfalme Abudullah II wa Jordan aliwaambia wanachama wa kamati ya Intelijensia na ile Uhusiano wa Kigeni ya Bunge la Seneti ya Marekani kuwa, sio sadfa kwamba kuna idadi kubwa ya magaidi miongoni mwa wakimbizi wanaokimbilia bara Ulaya na kwamba, mpango huo ni katika sera ya Rais Recep Teyyip Erdogan wa Uturuki ya kutuma magaidi barani Ulaya.

Mfalme huyo ameongeza kuwa, mbali na kuunga mkono makundi ya kigaidi nchini Syria, serikali ya Uturuki imeruhusu waasi wenye misimamo ya kufurutu ada kuvuka mpaka wa nchi hiyo na kuingia Syria, nchi hiyo ambayo imeshuhudiwa mapigano kwa takriban miaka mitano sasa, ambapo watu zaidi ya laki 4 na elfu 70 wamekwishauawa.

Aidha mfalme Abdullah II amedai kuwa nchi yake na Uingerea zinashirikiana kwa siri kuisaidia Kenya kukabiliana na kundi la kigaidi la Al Shabab.

Aidha amesema Jordan na Uingerea pia zimetuma vikosi vya kijeshi Libya kukabiliana na magaidi wa kundi la kitakfiri wa Daesh au ISIS.

Tovuti hiyo imemnukulu Mfalme Abdullah II wa Jordan akibainisha hayo wakati alipokutana na wabunge wa Baraza la Kongresi la Marekani mwezi Januari.

Mfalme huyo alidokeza kuwa nchi yake ina "kikosi cha haraka ambacho kitashirikiana na wanajeshi wa Uingereza na Kenya” ambacho kitaingia Somalia na kukabiliana na magaidi wa al Shabab.

Mfalme wa Jordan amenukuliwa akisema kuwa kuna haja ya kukabiliana na magaidi wa al Shabab kwani hivi sasa magaidi wa kundi hilo wanaelekea Libya na kujiunga na kundi la kigaidi la ISIS.

Serikali ya Kenya tayari imeshatuma wanajeshi zaidi ya 3,000 nchini Somalia tokea mwaka 2011 baada ya magaidi wa al-Shabab kutekeleza hujuma kadhaa ndani ya ardhi ya Kenya.

Magaidi wa al Shabab wameendeleza mashambulizi yao Kenya na pia kuwaua wanajeshi wa Kenya nchini Somalia ili kuishinikiza serikali ya Nairobi iondoe askari wake Somalia. Askari wa Kulinda Amani wa Umoja wa Afrika Somalia AMISOM wako nchini humo kuangamiza kundi la al Shabab na kuilinda serikali ya Somalia.

Katika wiki za hivi karibuni jeshi la Kenya limetangaza kuwaangamiza makumi ya magaidi wa al Shabab katika mapigano nchini Somalia.

3459396


captcha