IQNA

Wanawake Waislamu kutoka Iran, Misri washinda medali katika Taekwondo Olimpiki Rio

22:55 - August 20, 2016
Habari ID: 3470534
Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na Misri zimepata medali zao za kwanza za mashindano ya taekwondo ya wanawake katika michezo ya Olimpiki ya Rio, 2016.

Kwa mujibu wa mwandishi wa IQNA, wanawake wachanga kutoka nchi za Kiislamu ni nguvu ibuka katika taekwondo na hilo limebainika kufuatia mafanikia makubwa waliyopata katika michezo ya Olimpiki ya Rio di Janeiro nchini Brazil mwaka huu wa 2016.

Medali za shaba za Kimia Alizadeh Zenoorin wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na Hedaya Wahba wa Misri katika kategoria ya kila 57 siku ya Alhamisi ( 18 Agosti) ni ishara ya kuwepo vipaji katika nchi za Afrika Kaskazini na Magharibi mwa Asia (Mashariki ya Kati). Wanawake hao wawili walikuwa wa kwanza kupata medali za Olimpiki katika nchi hizo mbili katika mchezo wa Taekwondo huku Kimia Alizadeh akiwa mwanamke wa kwanza Muirani kuwahi kupata medali katika historia ya Olimpiki.

Kimia Alizadeh, mwenye umri wa miaka 18 aliweza kutwaa medali ya shaba baada ya kumshinda Nikita Glasnovic wa Sweden kwa pointi 5-1 na baada ya kushinda pambano lake la awali dhidi ya Phannapa Harnsujin wa Thailand kwa pointi 14-10.

"Natamani ningeweka historia kwa medali ya dhahabu... Namshukuru Mwenyezi Mungu nimeweza kuweka historia kwa medali ya shaba ili kufungua njia kwa wanawake wengine wa Kiirani", alisema Alizadeh.

"Nimepata msisimko mkubwa;na ninataka niwashukuru wazazi wangu na kocha wangu. Kwa kweli wamekuwa wakinipa msukumo ; na nimefurahi sana", ameongezea kueleza mwanamichezo huyo.


3460758
captcha