IQNA

Utawala wa Israel wapuuza azimio la UN na kuwajengea Wazayuni nyumba zaidi

22:45 - January 23, 2017
Habari ID: 3470809
IQNA- Utawala haramu wa Kizayuni wa Israel umeidhinisha ujenzi wa wa nyumba mpya 566 za walowezi wa Kizayuni katika mji wa Baitul Muqaddas Mashariki unaoukalia kwa mabavu kinyume cha azimio la Umoja wa Mataifa.

Uidhinishaji huo uliotangazwa Jumapili umefanyika siku mbili baada ya kuapishwa Donald Trump kuwa rais mpya wa Marekani, huku maafisa wa utawala wa Kizayuni wakieleza kwamba hatua hiyo ilikuwa imesitishwa kusubiri kumalizika kipindi cha utawala wa Barack Obama ambaye serikali yake imekuwa ikikosoa ujenzi wa vitongoji. Meir Turjeman, Naibu Meya wa Baitul Muqaddas inayokaliwa kwa mabavu amesema: "Kanuni za mchezo zimebadilika baada ya Donald Trump kuwa rais. Mikono yetu sasa haifungiki tena kama ilivyokuwa wakati wa Barack Obama. Hatimaye sasa tunaweza kujenga".Kwa mujibu wa Turjeman, maafisa wa utawala haramu wa Israel katika mji wa Baitul Muqaddas wamepitisha mipango ya ujenzi wa nyumba hizo ambao ulikuwa umeakhirishwa kwa ombi la Waziri Mkuu wa utawala huo ghasibu Benjamin Netanyahu katika kipindi cha mwezi uliopita wa Desemba wakati Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa lilipopitisha azimio la kuitaka Israel isitishe ujenzi wa vitongoji katika aradhi za Palestina unazozikalia kwa mabavu.

Naibu Meya wa Quds tukufu inayokaliwa kwa mabavu ameeleza pia kwamba mipango ya utoaji vibali vipya vya ujenzi wa nyumba nyingine 11,000 katika mji huo iko mbioni. Ujenzi wa vitongoji katika eneo la Ufukwe wa Magharibi linalokaliwa kwa mabavu ni hatua haramu kwa mujibu wa sheria za kimataifa. Hii ni katika hali ambayo baina ya mwaka 2009 na 2014 Israel imepanua kwa asilimia 23 ujenzi wa vitongoji katika eneo la Ufukwe wa Magharibi ikiwemo Baitul Muqaddas Mashariki. Hatimaye baada ya miaka kadhaa ya walimwengu kusubiri jibu la jamii ya kimataifa dhidi ya ujenzi haramu wa vitongoji vya walowezi wa Kizayuni katika ardhi zilizoporwa za Palestina, Disemba 23 Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa lilipasisha azimio nambari 2334 linaloitaka Israel isitishe mara moja ujenzi huo katika ardhi zilizoghusubiwa za Palestina.

Katika hatua isiyo ya kawaida, Baraza la Usalama la UN limepasisha azimio hilo kutokana na muswada uliopendekezwa na nchi nne za Malaysia, Venezuela, Senegal na New Zealand likilaani ujenzi wa vitongoji vya walowezi wa Kiyahudi katika ardhi zilizoghusubiwa za Palestina na kutaka ukomeshwe. Azimio hilo limepashwa na nchi 14 wanachama wa Baraza la Usalama mkabala wa kura moja tu ya Marekani ambayo imekataa kulipigia kura. 

Kwa mujibu wa azimio hilo, utawala haramu wa Israel unalazimika kusitisha mara moja na kikamilifu shughuli zote za ujenzi wa vitongoji vya walowezi wa Kiyahudi katika ardhi zote zinazokaliwa kwa mabavu za Palestina ikiwemo Quds Mashariki. Vilevile limesisitiza kuwa, ujenzi wa vitongoji vya walowezi katika ardhi ya Palestina unahatarisha sana mpango wa utatuzi wa mgogoro wa Palestina na ni kizuizi cha kurejeshwa amani.

3462006

captcha