IQNA

Kenya yaazimia kuimarisha utalii 'Halal'

15:59 - April 30, 2017
Habari ID: 3470962
TEHRAN (IQNA)-Kenya imeazimia kuimarisha utalii 'Halal' ambao unalenga kuwavutia watalii Waislamu kwa kutoa huduma ambazo zinazingatia mfundisho ya dini tukufu ya Kiislamu.

Waziri wa Utalii Kenya Najib Balala anasema: "Serikali imechukua hatua zote zinazohitajika kustawisha utalii Halal na tayari hatua zimeshachukuliwa kubuni sheria maalumu kwa ajili ya utalii huo."

"Tokea serikali hii iingie madarakani, imechukua hatua za kubuni sheria za utalii Halal na halmasharui husika zimeshapewa amri ya kutekeleza jambo hilo. Zamani tulikuwa tunapoteza watalii wengi, hasa kutoka nchi za Kiarabu, kwa sababu ya kukosa huduma halali lakini sasa tunaanzisha hoteli zenye kutoa huduma hizo. Aidha wafanyakazi wa hoteli hizo wanapewa mafunzo maalumu yanayohusu huduma Halal za kitalii," anasema waziri Balala.

Halikadhalika waziri huyo wa utalii Kenya anasema hoteli zenye kutoa huduma Halal kwa mfano zina sehemu tafauti za kuogelea za wanaume na wanawake na mfumo mzima wa upishi utazingatia kikamilifu chakula halali. Aidha hoteli zenye kutoa huduma kama hizo pia zimepangiwa kuwa sehemu maalumu za kuswali na hakutakuwa na ruhusa wa kuwa na pombe au tabia zisizo za Kiislamu katika hoteli hizo ili kuwavutia watalii Waislamu kutoka kote duniani. Aidha watalii wanofadhilisha kutekeleza ibada za Mwezi Mtukufu wa Ramadhani nchini Kenya watapata huduma maalumu za mwezi huo katika hoteli zenye huduma za Halal.

Balala amesisitiza kuwa serikali ya sasa ya Kenya inalipa umuhimu mkubwa suala la hisia za Waislamu kuliko wakati wowote ule.

Kwa upande wake, Mohammad Hersi, Mkuu wa Jumuiya ya Utalii ya Eneo la Pwani, Mohammad Hersi anasema kutokana na turathi ya Kiislamu katika eneo la pwani nchini Kenya, eneo hilo linaweza kuwa kivutio kikubwa kwa watalii Waislamu wanaotaka huduma Halal.

Amongeza kuwa: "Sekta ya utalii Halal inastawi kwa kasi zaidi duniani huku takwimu zikionyesha kuwa Waislamu wanaoenda safari za kitalii wanazidi kuongezeka: Kwa mfano mwaka 2015, Kenya ilipokea watalii 40,875 kutoka Umoja wa Falme za Kiarabu ikiwa ni ongezeko kubwa ikilinganishwa na mwaka kabla yake wakati tulipata watali 24,828 kutoka nchi hiyo."

Mwezi Februari mwaka huu, Halmashauri ya Kuratibu Utalii nchini Kenya TRA imesema imeandaa sheria za kutoa vibali vya 'Halal' kwa ajili maeneo ya kitalii yanayolenga kuwahudumia watalii Waislamu wanaotaka huduma kwa msingi wa mfundisho ya Kiislamu.

Mkurugenzi Mkuu waTRA Lagat Kipkorir alisema viwango vya utalii Halal vinatayarishwa kwa ushuhirikiano na Idara ya Viwango Kenya. "Tumetayarisha mpango wa kina kutunga kanuni, kuwashirikisha washikadau, kudhamini viwango, na mafunzo kabla ya kuzindua rasmi utalii Halal," alisema Kipkorir.

3594523
captcha