IQNA

Sayyed Hassan Nasrallah

Saudia ilimchochea Waziri Mkuu wa Lebanon Saad Hariri kujiuzulu

14:31 - November 06, 2017
Habari ID: 3471250
TEHRAN (IQNA)-Katibu Mkuu wa Harakati ya Hizbullah ya Lebanon, Sayyid Hassan Nasrallah amesema, kujiuzulu Saad Hariri kama Waziri Mkuu wa Lebanon ni uamuzi ambao ulilazimishwa na utawala wa Saudi Arabia.

Nasrallah aliyasema hayo jana jioni ya Jumapili katika hotuba aliyoitoa mjini Beirut, mji mkuu wa Lebanon baada ya kujiuzulu Hariri. Ameongeza kuwa, Hariri alitakiwa afike Riyadh na hapo wakuu wa Saudia wakamlazimisha kujiuzulu na wakamuandikia barua yake ya kujiuzulu watakavyo wao.

Katibu Mkuu wa Hizbullah amesema kujiuzulu Hariri kunaonyesha namna Saudi Arabia inavyoingilia masuala ya ndani ya Lebanon.

Sayyid Hassan Nasrallah amesema Hizbullah haikutaka Hariri ajiuzulu na kwamba kujiuzulu kwake kunakiuka mamlaka ya kujitawala, izza na heshima ya Lebanon.

Sayyid Nasrallah ameashiria suala la kwenda sambamba kujiuzulu kwa Hariri na  kukamatwa wanawafalme kadhaa nchini Saudia na kusema: "Suali linaloulizwa hapa ni hili kuwa, je, tunaweza kutizama kujiuzulu Hariri kama sehemu ya vita na malumbano ndani ya Saudia na eneo la Mashariki ya Kati?

Katibu Mkuu wa Hizbullah ya Lebanon amesisitiza udharura wa kulinda amani na utulivu wa Lebanon na kuongeza kuwa: "Nawaaambia Walebanon wasiwe na wasiwasi na wote waende kwa mujibu wa mantiki na akili na wasitafakari kurejea katika mazingira ya zamani ya malumbano ya kikaumu na kimadhehebu."

Vilevile ameashiria madai ya kuwepo njama za kutaka kumuua kabla hajajiuzulu na kusema: "Moja ya sababu ya kanali ya Saudia ya Al Arabiya  kudai kuwa kulikuwa na njama za kumuua Saad Hariri ni kumzuia kurejea Lebanon."

Katibu Mkuu wa Hizbullah ameashiria pia uvumi wa Israel kuanzisha vita dhidi ya Lebanon baada ya kujiuzulu Hariri na kusema: "Waisraeli hawataingia katika vita na Lebanon isipokuwa tu wawe na yakini watapata ushindi mutlaki katika vita hivyo."

3464342


captcha