IQNA

Rais wa Nigeria atakiwa amuachilie huru kiongozi wa Harakati ya Kiislamu

20:34 - November 10, 2017
Habari ID: 3471256
TEHRAN (IQNA)-Rais Muhammadu Buhari wa Nigeria ametakiwa amuachilie huru kiongozi wa Harakati ya Kiislamu nchini humo Sheikh Ibrahim Zakzaky ambaye anashikiwa kwa miaka miwili sasa bila kufunguliwa mashtaka baada ya wanajeshi kuvamia makao yake na kumjeruhi vibaya.

Katika barua kwa Rais wa Nigeria siku ya Alhamisi, wakili mtetezi wa haki za binadamu Femi Falana amesema Sheikh Zakzaky na mke wake wanapaswa kuachiliwa huru kwa sababu za kiafya.

Itakumbukwa kuwa Sheikh Ibrahim Zakzaky akiwa na mke wake walitekwa nyara na Jeshi la Nigeria mwezi Disemba mwaka 2015 wakati askari walipovamia kituo chake cha kidini huko katika mji wa Zaria jimboni Kaduna. Tokea wakati huo Sheikh Zakzaky na mkewe wamekuwa wakizuiliwa katika mojawapo ya vituo vya kijeshi vya nchi hiyo bila kufunguliwa mashktaka.

Uvamizi huo ulijiri baada ya Jeshi la Nigeria kudai kuwa wafuasi wa Harakati ya Kiislamu ya Nigeria walikuwa na njama ya kutaka kumuua mkuu wa jeshi hilo, madai ambayo yalikanushwa vikali na wafuasi wa harakati hiyo.

Inakadiriwa kuwa Waislamu 1000 wasio na hatia waliuawa katika tukio hilo huku Sheikh Zakzaky, ambaye hali yake ya kiafya si nzuri, akiendelea kushikiliwa korokoroni pasina kufunguliwa mashtaka.

Wakili Femi Falana anasema Sheikh Zakzaky anaelekea kupoteza uwezo wa kuona macho yote mawili kutokana na mateso anayopata mikononi mwa wanajeshi wa Nigeria. Aidha amesema hali ya kiafya ya mke wa mwanazuoni huyo nayo si nzuri hata kidogo.

Falana ambaye ni wakili mashuhuri anasema amefanikiwa kumtembelea Sheikh Zakzaki na mkewe katika eneo la siri wanaokoshikiliwa na vikosi vya usalama katika mji mkuu Abuja na kwamba hali ya wawili hao si nzuri. Aidha amesema hali ya mke wa Sheikh Zakzaky ni mbaya sana. Amesema mke wa Sheikh Zakzaky alipigwa risasi wakati wa hujuma ya Desemba 2015 na risasi hizo zingali ndani ya mwili wake huku Idara ya Usalama wa Taifa Nigeria ikikataa kumpa matibabu hivyo ana maumivu makali yanayomsumbua kila siku.

3471056/

captcha