IQNA

Sayyid Hassan Nasrallah

Saudia kumkamata Waziri Mkuu wa Lebanon Rafiq Hariri ni kitendo cha vita

18:49 - November 11, 2017
Habari ID: 3471257
TEHRAN (IQNA)-Sayyid Hassan Nasrallah, Katibu Mkuu wa Hizbullah ya Lebanon, amesema kujiuzulu Waziri Mkuu wa nchi hiyo Saad Hariri kumetokana na kulazimishwa na utawala wa Saudi Arabia na kubainisha kwamba: muamala wa udhalilishaji aliofanyiwa Waziri Mkuu wa Lebanon na utawala wa Aal Saud ni sawa na kuwadhalilisha Walebanon wote.

Katibu Mkuu wa Hizbullah aliyasema hayo jana katika hotuba aliyotoa kwenye viunga vya mji mkuu wa Lebanon, Beirut kwa mnasaba wa Arubaini ya Imam Hussein AS na "Siku ya Shahidi wa Hizbullah". Sayyid Hassan Nasrallah amefafanua kwamba: amani na uthabiti usio na mfano ulikuwa umetawala nchini Lebanon; na wananchi walikuwa katika hali ya utulivu, lakini kuanzia Jumamosi iliyopita Lebanon imetumbukizwa kwenye lindi la mgogoro wa kisiasa.

Katibu Mkuu wa Hizbullah ameongeza kuwa Saudia imeitangazia vita Lebanon kwa kumweka kizuizini Waziri Mkuu wa nchi hiyo na kumlazimisha ajiuzulu.

Saudia imemlazimisha Hariri ajiuzulu

Sayyid Hassan Nasrallah amebainisha kuwa: leo wananchi wa Lebanon na dunia wana hakika kwamba Saudi Arabia imemlazimisha Saad Hariri ajiuzulu na kumweka kwa nguvu ndani ya nchi hiyo; Hariri amewekwa kizuizini nchini Saudi Arabia na kuzuiwa asirudi Lebanon; na utawala wa Aal Saud unafanya kila njia kulazimisha mtu mwengine mpya awe Waziri Mkuu wa Lebanon.

Katibu Mkuu wa Hizbullah amesisitiza kwamba: kujiuzulu kwa Saad Hariri kumefanyika kinyume cha sheria na kwa kulazimishwa; na serikali iliyoko Lebanon ingali ni serikali halali. Ameongeza kuwa taarifa ya kujiuzulu Hariri pia imeandikwa na utawala wa Riyadh.

Nasrallah aidha amefichua kwamba Saudia imefikia hatua hata ya kuuomba utawala wa Kizayuni wa Israel uanzishe mashambulio ya kijeshi dhidi ya Lebanon kwa kisingizio cha kupambana na Hizbullah na kwamba tayari imeshatumia mabilioni ya dola kwa ajili ya kufikia lengo hilo.

"Saudia inataka kuiteketeza Lebanon kwa kisingizio cha kupambana na Hizbullah. Ilikuwa ndio mpangaji mkuu wa vita vya mwaka 2006 dhidi ya Lebanon", amesema Katibu Mkuu wa Hizbullah.

Wito wa Rais wa Lebanon

Wakati huo huo Rais Michel Aoun wa Lebanon ametoa wito kwa mataifa mengine ya dunia yaishinikize Saudi Arabia ili iweze kujulikana hatima ya kisiasa ya Saad Hariri, Waziri Mkuu wa Lebanon aliyetangaza kujiuzulu wadhifa wake huo.

Siku ya Jumamosi iliyopita ya tarehe 4 Novemba, Saad Hariri alitangaza kujiuzulu uwaziri mkuu wa Lebanon kupitia taarifa aliyoisoma akiwa mjini Riyadh, Saudi Arabia. Licha ya kupita wiki moja sasa, Hariri bado hajarudi nchini kwake Lebanon. Baadhi ya duru zinaripoti kuwa utawala wa Aal Saud unatoa mashinikizo kwa ukoo wa Hariri ufanye mageuzi ya kumweka Bahaa Hariri, kaka wa Saad Hariri katika uongozi wa harakati ya Al-Mustaqbal badala ya waziri mkuu huyo wa Lebanon aliyetangaza kujiuzulu.

Kuwekwa kizuizini au kupatiwa ukaazi wa lazima Saad Hariri nchini Saudi Arabia ni hatua inayokinzana waziwazi na taratibu za sheria za kimataifa.

3464381


captcha