IQNA

Rais wa Uturuki amwambia Bin Salman wa Saudia, Uislamu si Milki yako

10:59 - November 12, 2017
Habari ID: 3471259
TEHRAN (IQNA)- Rais Reccep Tayyip Erdogan wa Uturuki amekosoa vikali matamshi Mrithi wa Kiti cha Ufalme Saudia Mohammad Bin Salman kuhusu kile alichodai kuwa ni "Uislamu wa misimamo ya wastani."

Akizungumza katika Ofisi ya Rais mjini Ankara, Erdogan amesema Uislamu unaotajwa kuwa ni wa misimamo wa wastani ni Uislamu unaopigiwa debe na nchi za Magharibi. Ameongeza kuwa kimsingi, katika Uislamu hakuna Uislamu wa Wastani na Uislamu usio wa Wastani.

Mwezi jana Bin Salman aliapa kurejesha kile alichodai kuwa ni Uislamu wa wastani katika Ufalme wa Saudia ambao unafuata pote la Uwahhabi ambao umekuwa chanzo cha misimamo mikali na ugaidi kote duniani.

Akizungumza Ijumaa katika kikao cha Baraza la Ushauri wa Wanawake la Jumuiya ya Ushirikiano wa Nchi za Kiislamu OIC, Erdogan alimuashiria kwa njia isiyo ya moja kwa moja Bin Salman na kusema: "Mtu anayeeneza mtazamo huu anadhani yeye anaumiliki Uislamu. La hasha, Uislamu si milki yako."

Pamoja na hayo, weledi wa mambo wanasema, jibu kali alilotoa Erdogan kwa Bin Salman linatokana na hitilafu za kina baina ya Saudi Arabia na Uturuki katika miezi ya hivi karibuni.

Hitilafu baina ya Saudia na Uturuki zilikuwepo kwa muda mrefu lakini mgongano baina ya nchi hizo mbili umedhihirika wazi zaidi katika miezi ya hivi karibuni. Ugomvi wa Ankara na Riyadh hivi sasa unatokana na msuguano uliopo baina ya Qatar na Saudi Arabia na waitifake wake. Uturuki imechukua msimamo wa wazi wa kuunga mkono Qatar katika mgogoro huo wa Ghuba ya Uajemi na hilo limepelekea Erdogan ahasimiane na watawala wa Saudia na waitifaki wao.

Tokea mgogoro huo wa Qatar uanze Juni, viongozi wa Uturuki na Saudia wamekuwa wakikosoana na kurushiana vijembe mara kwa mara huku kila moja akitaka kujionyesha kuwa mbabe.


3464387

captcha