IQNA

Mashindano ya Kimataifa ya Qur’ani ya Wanawake yaanza Dubai

10:11 - November 13, 2017
Habari ID: 3471262
TEHRAN (IQNA)- Duru a pili ya Mashindano ya Kimataifa ya Qur’ani Tukufu ya Wanawake yameanza Jumapili mjini Dubai katika Umoja wa Falme za Kiarabu (UAE).

Mashindano hayo ambayo ni maarufu kama Mashindano ya Qur’ani ya Sheikha Fatima Bint Mubarak yanafanyikia baina ya tarehe 12-24 Novemba ambapo yatakuwa yakifanyika kila siku katika awamu mbili, ya asubuhi kuanzia saa nne hadi saa saba na kisha kuanzia saa kumi na mbili jioni hadi saa tatu usiku. Mashindano hayo yanafanyika katika ukumbi wa Jumuiya ya Sayansi na Utamaduni katika eneo la Mamzar.

Mashindano ya Qur’ani ya Sheikha Fatima Bint Mubarak yanafanyika kwa himaya ya Sheikh Mohammed bin Rashid al Maktoum, Makamu wa Rais na Waziri Mkuu wa UAE ambaye pia ni mtawala wa Dubai.

Mkuu wa jopo la majaji Abdullah bin Mohammed Al Jarallah amesema kuna washiriki 75 kutoka maeneo yote duniani na wanatumia mbinu za qiraa za Hafs, Warsh na Qaloon.

Amesema majaji ni wataalamu na wanazuoni wa Qur’ani na pia watatumia teknolojia za kisasa katika kubaini washiriki bora katika mashindano hayo.

Kati ya nchi zinazoshiriki katika mashindano hayo ni pamoja na Nigeria, Pakistan, Marekani, Maldives, Norway, Chad, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, Misri. Afrika Kusini, Uingereza na Benin.

Mwaka jana nafasi ya kwanza katika mashindano hayo ilishikwa kwa pamoja na Zahra Hani from Algeria and Zakiya Abu Bakr Mahmoud Ilmi wa msumbiji.

Walifuatiwa kwa taratibu na wawakilishi wa Qatar, Afghanistan, Norway, Umoja wa Falme za Kiarabu, Pakistan, Niger, na Bangladesh. Mshiriki wa Iran, Hannaneh Khalafi, aliyekuwa na umri wa miaka tisa, alishika nafasi ya 10 kwa pamoja na Amina Jafar wa Nigeria.

3464405

captcha