IQNA

Isa Masih AS (Yesu) katika Uislamu

9:55 - December 26, 2017
Habari ID: 3471325
TEHRAN(IQNA)- Disemba 25 inasadifiana na siku aliyozaliwa Nabii Isa Masiih (as) kwa mujibu wa imani ya Wakristo waliowengi.

Mtume huyo mwema alikuwa mtoa bishara njema na mlinganiaji wa kweli na upendo na itikadi na Mungu Mmoja. Isa Masiih alizungumza kwa amri ya Mwenyezi Mungu akiwa katika susu na kuwaambia watu waliokuwa katika mghafala wa zama hizo kama inavyotwambia aya ya 30 hadi 33 za Suratu Maryam kwamba: Na akasema: Hakika mimi ni mja wa Mwenyezi Mungu, amenipa kitabu na kunifanya Nabi. Na amenijaalia ni mwenye kubarikiwa popote pale niwapo na ameniusia Swala na Zaka maadamu ni hai. Na kumtendea wema mama yangu. Wala hakunifanya jeuri, muovu. Na amani iwe juu yangu siku niliyozaliwa, na siku nitakayokufa, na siku nitakayofufuliwa."

Wakati wa kuzaliwa

Nabii Isa alizaliwa katika zama ambazo makundi mbalimbali ya Kiyahudi yalikuwa yamezama katika hitilafu na migawanyiko mikubwa. Makundi mawili makuu ya Wasadukayo (Sadducees) na Mafarisayo (Pharisees) yalikuwa yakidhibiti na kutawala itikadi za watu wa zama hizo. Wasadukayo (Sadducees) lilikuwa kundi la mabwanyenye na aghlabu yao walikuwa makuhani na wanazuoni wa kidini ambao walikuwa wakishirikiana na utawala wa kifalme wa Roma kwa ajili ya kulinda mafundisho na ada za kidini na hawakukabiliana kwa njia yoyote ile ya utamaduni wa Kigiriki. Hii ni kwa sababu walikuwa wakiamini kwamba, Mwenyezi Mungu pia ameeneza maadili ya Kitabu Kitakatifu kati ya wasio Wayahudi. Mkabala wake, Mafarisayo (Pharisees) lilikuwa kundi lisilo la makuhani lakini lenye ushawishi mkubwa zaidi kuliko Wasadukayo (Sadducees). Kundi hili liliamini kuwa, kaumu ya Mayahudi inapaswa kuwa kaumu tofauti na iliyojitenga na kaumu nyinginezo na haipasi kufuata kaumu hizo au kuchanganyika nazo. Kundi la Mafarisayo (Pharisees) lilikuwepo katika maeneo yote ya Palestina na lilidhibiti masinagogi na maabadi zote za nje ya Baitul Muqaddas (Jerusalem) ambako Wayahudi walikuwa wakikusanyika kwa ajili ya ibada au kusoma. 

Mbali na makundi hayo mawili makuu, kulikuwepo makundi mengine kama Samaritans (Wasamaria) na kundi na Wayahudi wenye misimamo mikali lililokuwa maarufu kama Zealots. Wasamaritani katika mtazamo wa makundi mengine, walitambuliwa kuwa makafiri, na Zealots lilikuwa kundi la Wayahudi wenye misimamo ya kuchupa mipaka la kisiasa lililokuwa likiwachochea Wayahudi kuwafukuza kwa mabavu na kwa njia za mauaji ya kigaidi Warumi na utawala wao katika ardhi ya Palestina. Kundi hili halikushambulia Warumi pekee, bali hata Wayahudi wenzao ambao kwa madai yao, hawakuwa na ghera ya kutosha ya udini na utaifa. 

Utabiri uliopuuzwa na Mayahudi

Nabii Isa Masih alizaliwa katika mazingira kama haya. Wakuu wa kaumu ya Mayahudi katika kila kundi walijua vyema sifa na alama zake kutokana na utabiri wa hapo kabla na habari walizosoma na kukusanya katika vitabu vya kale. Hata hivyo walipuuza utabiri na alama hizo tangu hapo mwanzoni na kukabiliana na Nabii huyo mkubwa wa Mwenyezi Mungu. Hatua ya kwanza kabisa ya Mayahudi hao ilikuwa kumtuhumu mama yake Masih, Bibi Maryam (as) kuwa ni fasiki ili wapate kumrujumu kadamnasi. Hata hivyo njama hiyo ilifeli, na Isa na mama yake, Bibi Maryam wakaokoka kifo na vitimbi vya Mayahudi baada ya Masih kuzungumza akiwa kwenye susu na kusema: "Hakika mimi ni mja wa Mwenyezi Mungu, amenipa kitabu na akanijaalia kuwa Nabi..".

Nabii Isa (as) alibaathiwa na kuamrishwa kutangaza ujumbe wa Mwenyezi Mungu baina ya Banii Israel akiwa na umri wa karibu miaka 30. Alifanya jitihada kubwa za kuwaongoza katika kweli na haki na kuwaondoa katika upotovu. Aliwabainishia halali na haramu na kuwahalalishia mengi waliyokuwa wamekatazwa. Kwa mujibu wa Injili ya Mathayo 4/17 ni kwamba Isa alianza kuhubiri kwa kusema: “Tubuni, kwa sababu Ufalme wa mbinguni umekaribia.”

Kuwaongoza watu katika njia ya haki

Mbali na kuwaongoza watu katika njia ya haki, Nabi Isa alikuwa akitibu wagonjwa. Alikuwa akitibu vipovu na barasi au mbalanga na kufufua wafu kwa uwezo wake Mola Muumba. Vilevile alikuwa akitengeneza ndege kutoka kwenye udongo. Daima alikuwa msaidizi wa watu waliokuwa wakidhulumiwa na kukandamizwa na aliwakirimu na kuwafanyia ihsani sana watoto na wanawake. Wakati huo huo alipinga vikali sheria kali za baadhi ya Mafarisayo (Pharisees) na misimamo ya kuchupa mipaka ya Zealots. 

Nabi Isa (as) alipata mashaka na tabu kubwa katika kuwaongoza Wayahudi na kuwaelekeza katika njia sahihi. Katika mashaka hayo alielewa kwamba, Wayahudi wanashikilia maasi na hawakuwa tayari kuachana na dhambi na njia potovu. Alisimama katika kaumu yake na kusema: "Nani kati yenu atakayenisaidia katika njia ya Mwenyezi Mungu?" Watu wachache kati ya Mayahudi walijitokeza na kuitikiwa wito wake. Kundi hilo lilikuwa na watu wasafi ambao Mwenyezi Mungu SW anawataja katika Qur'ani tukufu kwa jina la "Hawariyyun". Kundi hili la Hawariyyun lilitangaza utayarifu wao wa kumsaidia Nabi Isa Masih katika njia ya Mwenyezi Mungu kama inavyosimilia Qur'ani tukufu katika aya ya 52 hadi 53 za Suratu Aal Imran zinazosema: "Isa alipohisi kuwa kati yao pana ukafiri alisema: Nani wasaidizi wangu kwa Mwenyezi Mungu? Wanafunzi wake wakasema: Sisi ni wasaidizi wa Mwenyezi Mungu. Tumemwamini Mwenyezi Mungu, na shuhudia kwamba, sisi hakika ni Waislamu. Mola wetu Mlezi! Tumeyaamini uliyoyateremsha, na tumemfuata huyu Mtume, basi tuandike pamoja na wanaoshuhudia."

Nabii Isa AS hakuvumilia ufisadi

Isa na wanafunzi wake hao walielekea katika maeneo ya kaskazini mwa Palestina na kuwafundisha watu dini halisi ya Mwenyezi Mungu. Maarifa ya dini yaliyofundishwa na Nabi Isa yaliwashangaza wengi na kuwakasirisha wanasiasa waliokuwa wakitawala jamii. Hii ni kutokana na ukweli kwamba, Nabii huyo mwema wa Mwenyezi Mungu alipinga vikali tabia ya watawala na makuhani wa duini ya Kiyahudi ya kuzama katika anasa na dunia. Hakuvulimia ufuska na ufisadi wa aina yoyote na kwa msingi huo makundi yote ya Wayahudi yalianza kumkadhibisha na kumpiga vita. Makundi hayo yalitayarisha uwanja na mazingira ya kumuua mjumbe huyo mwema wa Allah SWT. Ili kufikia lengo hilo chafu, Mayahudi hao walimchochea Kaizari wa Roma na kumwambia: Kama hali hii itaendelea, ufalme wako pia utatoweka, hivyo ili kulinda utawala na ufalme wako huna budi kumuua Masia!

Isa Masih aling'amua njama yao na akajificha katika shamba moja akiwa pamoja na Hawariyyun na wanafunzi wake. Hata hivyo mtu mmoja kati ya wanafunzi wake aliyejulikana kwa jina la Yuda aliwaonesha maadui mahali lipokuwa amejificha. Maafisa wa utawala walivamia eneo hilo nyakati za usiku na kulizingira. Wanafunzi wa Isa Masih walipohisi hatari walimkimbia na kumuacha peke yake, lakini Mwenyezi Mungu SWT kamwe hakumuacha peke yake Mtume wake mwema katika kipindi hicho hatari. Mwenyezi Mungu SWT alimlinda Mtume wake na kumdhihirisha Yuda aliyekuwa akifanya ujasusi dhidi ya Nabii huyo katika sura ya Isa, na maadui wakamkamata yeye wakidhani kuwa ni Masih. Yuda alichanganyikiwa kutokana na hofu na machungu mengi na hatimaye akashindwa kuzungumza na kujiarifisha.

Nabii Isa AS hakusulibiwa

Hata wakati alipoweza kufungua mdomo na kuzungumza, hakuna mtu aliyekuwa tayari kukubali maneno yake. Yuda alipandishwa msalabani na kusulubiwa.Watu walioshuhudia tukio hilo wote walidhani kuwa Isa Masih ameuawa, lakini kama inavyosisitiza Qur'ani tukufu, Nabii huyo mwema wa Mwenyezi Mungu hakusulubiwa wala kuuawa. Aya za 157 na 158 za Suratu Nisaa zinasema: Na kwa kusema kwao: Sisi tumemuuwa Masih Isa, mwana wa Maryamu, Mtume wa Mwenyezi Mungu -, nao hawakumuuwa wala hawakumsalibu, bali walifananishiwa tu. Na hakika waliokhitalifiana katika haya wamo katika shaka nayo. Wao hawana ujuzi nayo wowote, ila ni kufuata dhana tu. Wala hawakumuuwa kwa yakini. Bali Mwenyezi Mungu alimwinua kwake, na hakika Mwenyezi Mungu ni Mwenye nguvu, Mwenye hikima"

 

3464769

captcha