IQNA

Tarjumi ya kwanza ya Qur'ani kwa lugha ya Kirundi yazinduliwa Burundi

14:06 - December 27, 2017
Habari ID: 3471326
TEHRAN (IQNA)-Tarjumi ya kwanza ya Qur'ani kwa lugha Kirundi imezinduliwa nchini Burundi katika hatua ambayo imetajwa kuwa kihistoria tokea Uislamu uingie nchini humo.

Sheikh Sadiki Kajandi, mwenyekiti wa Baraza la Kiislamu Burundi (COMIBU) amesema,"Hili ni tukio kubwa kwetu. Tumepokea tarjama ya kwanza ya Qur'ani kwa lugha ya Kirundi na hii ni mara ya kwanza tokea Uislamu uingie Burundi."

Mradi huo wa tarjumi ya Qur'ani umetekelezwa na Jumuiya ya Waislamu ya AMES na ni kazi iliyodumu kwa muda wa miaka minane. Mwenyekiti wa Ames Sheikh Abdi Habonimana amesema walitembelea mikoa yaote ya Burundi ili kupata maoni ya Waislamu kuhusu maneno na misimiati iliyotumiwa katika tarjama hiyo. "Tunawashukuru Waislamu na wasio kuwa Waislamu, wakiwemo wahadhiri wa vyuo vikuu, ambao wametoa mchango wao katika tarjumi hii ya Qur'ani ya Kirundi."

Lugha ya Kirundi inazungumzwa Burundi, maeneo ya Tanzania, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo na Uganda. Waisalmu wanakadiriwa kuwa ni asilimia 10 ya watu wote milioni 10 nchini Burundi.

Kuna jamii kubwa ya Waislamu katika mji mkuu wa Burundi, Bujumbura wakiwemo Wafanya biashara kutoka Senegal, Niger, Guinea na Mali. Aidha kuna jamii ya Waislamu Waarabu na Wahindi. Kwa mujibu wa nyaraka za historia, Uislamu uliwasili Burundi mwanzoni mwa karne ya 19.

3676652

captcha