IQNA

Sheikh Zakzaky wa Nigeria aonekana hadharani kwa mara ya kwanza tokea 2015

11:21 - January 14, 2018
Habari ID: 3471354
TEHRAN (IQNA)- Sheikh Ibrahim Zakzaky, Kiongozi wa Harakati ya Kiislamu ya Nigeria ambaye kwa miaka miwili sasa anashikiliwa kinyume cha sheria, kwa mara ya kwanza jana alionekana hadharani alipohojiwa na waandishi habari.

Sheikh Zakzaky amehojiwa na vyombo vya habari huku akiwa na kifaa cha kitiba  shingoni ambacho aghalabu hutumiwa na watu wenye maumivu shingoni. Akizungumza na waandishi habari akiwa katika ofisi za Idara ya Usalama wa Taifa (DSS) katika mji mkuu wa Nigeria, Abuja, Sheikh Zakzaky ambaye amekuwa akishikiliwa kinyume cha sheria pasina kufunguliwa mashtaka hata baada ya mahakama kuamuru aachiliwe huru, alisema kwa mara ya kwanza ameruhusiwa kumuona daktari wake binafsi huku akiwashukuru wote waliomkumbuka katika dua. Amesema Jumatatu iliyopita hali yake ilizoorota lakini akaanza kupata afueni baada ya kuruhusiwa kuona madaktari wake binafsi. Amesema alikataa kupata matibabu ya madkatari wa Idara ya Usalama na kwa msingi huo hatimaye madaktari wake binafsi waliruhusiwa kumpa matibabu. Sheikh Zakzaky ameonekana hadharani baada ya kuenea uvumi kuwa amefariki, uvumi ambao ulikanushwa vikali na wakili wake, Femi Falana.

Itakumbukwa kuwa Sheikh Ibrahim Zakzaky akiwa na mke wake walitekwa nyara na Jeshi la Nigeria mwezi Disemba mwaka 2015 wakati askari walipovamia kituo chake cha kidini huko katika mji wa Zaria jimboni Kaduna. Tokea wakati huo Sheikh Zakzaky na mkewe wamekuwa wakizuiliwa katika mojawapo ya vituo vya kijeshi vya nchi hiyo bila kufunguliwa mashktaka.

Uvamizi huo ulijiri baada ya Jeshi la Nigeria kudai kuwa wafuasi wa Harakati ya Kiislamu ya Nigeria walikuwa na njama ya kutaka kumuua mkuu wa jeshi hilo, madai ambayo yalikanushwa vikali na wafuasi wa harakati hiyo.

Inakadiriwa kuwa Waislamu 1000 wasio na hatia waliuawa katika tukio hilo huku Sheikh Zakzaky, ambaye hali yake ya kiafya si nzuri, akiendelea kushikiliwa korokoroni pasina kufunguliwa mashtaka.

3464935

captcha