IQNA

Qur'ani Tukufu ni muongozo kwa wanadamu wa zama zote

16:21 - March 29, 2018
Habari ID: 3471447
TEHRAN (IQNA)- Mhadhiri wa Uislamu kutoka India amesema Qur'ani Tukufu ni muongozo kamili kwa wanadamu wa zama zote.

"Qur'ani Tukufu inalipa umuhimu mkubwa suala la heshima ya mwanadamu. Utamaduni wote wa Uislamu uko katika Msingi wa Qur'ani Tukufu," amesema Profesa Obaidullah Fahad Mwenyekiti wa Kitengo cha Masomo ya Kiislamu katika Chuo Kikuu cha Waislamu cha Aligarh cha India wakati akizungumza nchini Pakistan katika kongamano la 'Ubunifu katika Ustaarabu na Utamaduni wa Kiislamu."

Mwanazuoni huyo wa India amesema kuheshimu wanawake, nidhamu, usalama, maelewano na usawa ni kati ya nukta ambazo zimesisitizwa katika mafundisho ya Qur'ani. "Tunapaswa kuwa na nidhamu katika Dhahiri na pia katika batini na hilo liakisiwe katika fikra na vitendo vyetu. Hakuna ustaarabu unaoweza kustawi kwa msingi wa fikra  hasi…hivyo tunapaswa kuwa na fikra chanya kwani nukta hii ni muhimu katika maisha yetu," amesema.

Akizungumza katika kikao hicho, Profesa Zia ul-Haq, Mkurugenzi wa Kituo cha Utafiti wa Kiislamu cha Chuo Kikuu cha Kimataifa cha Kiislamu cha Islamabad ameashiria nadharia ya Allama Iqbal wa Pakistan kuhusu kuhuishwa ustaarabu wa Kiislamu na kusema Waislamu wamepuuza utamaduni wao asili. Ametaka vijana wawe na nafasi muhimu katika kuhuisha ustaarabu halisi wa Kiislami ili nchi za Kiislamu ziweza kuwa na utambulisho sahihi.

3465466

captcha