IQNA

TV ya Qur'ani ya Iran kurusha mubashara mashindano ya kimataifa ya Qur'ani

12:02 - April 19, 2018
Habari ID: 3471471
TEHRAN (IQNA)- Kanali ya Televisheni ya Qur'ani ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran itarusha mubashara au moja kwa moja Mashindano ya 35 ya Kimataifa ya Qur'ani yanayoanza Alhamisi hii mjini Tehran.

Kwa mujibu wa Idara ya Mahusiano ya Umma ya Kanali hiyo, mashindano hayo yatakuwa yakirushwa hewani mubashara asubuhi na jioni.

Kanali hiyo pia itarusha mubashara sherehe za ufunguzi wa mashindano hayo, leo Aprili 19 na sherehe za kufunga, Aprili 25. Halikadhalika TV ya Qur'ani ya Iran itakuwa na vipindi maalumu vya Qur'ani vitakavyowajumuisha wanazuoni na washiriki wa mashindano ya Kimataifa ya Qur'ani ya Iran.

Mkuu wa Shirika la Wakfu la Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema miji mitatu nchini itakuwa mwenyeji wa mashindano kadhaa ya kimataifa ya Qur'ani. Unaweza kuitazama TV ya Qur'ani ya Iran mubashara kwa kubonyeza hapa.

Sherehe za Ufunguzi zitaanza saa tisa unusu hadi saa moja unusu kwa saa za Afrika Mashariki.

Hali kadhalika kuanzia Ijumaa 20 Aprili hadi Jumatano 25 Aprili mashindano hayoyatakuwa yakirushwa hewani kila siku kuanzia saa tatuu asubuhi hadi saa  saba kwa saa za Iran sawa na saa moja na nusu asubuhi hadi saa tano na nusu mchana kwa saa za Afrika Mashariki. Wakati wa Alasiri mashindano hayo yatakuwa yakianza saa kumi hadi saa mbili  usiku kwa saa za Iran sawa na saa nane unusu hadi saa kumi na mbili unusu kwa saa za Afrika Mashariki

Akizungumza na waandishi habari mjini Tehran Jumatatu, Mkuu wa Shirika la Wakfu la Iran Hujjatul Islam Ali Mohammadi amesema mashindano ya kimataifa ya Qur'ani ya Iran mwaka huu yatafanyika katika miji mitatu ya Tehran, Qum na Mashhad.

Ameongeza kuwa mashindano hayo yatakuwa na wageni 370 kutoka nchi mbali mbali duniani wakiwemo watakaoshindano, majaji na wageni wengine waalikwa.

Kwa mujibu wa Sheikh Mohammadi,  mwaka huu mashindano ya Qur'ani yatakuwa na washiriki kutoka nchi 84 na yanatazamiwa kuanza rasmi Aprili 19 hapa mjini Tehran.

Amesema mashindano ya mwaka huu yatajumuisha Mashindano ya 35 ya Kimataifa ya Qur'ani Tukufu ya Iran (ya kawaida maalumu kwa ajili ya wanaume) na pia kutakuwa na mashindano mengine ya Qur'ani ya wanawake, ya wenye ulemavu wa macho, ya wanafunzi wa shule na ya wanachuo wa vyuo vya kidini.

3706876

captcha