IQNA

Hizbullah yapongeza Malaysia kwa kujiondoa katika muungano wa kivita wa Saudia

10:38 - June 30, 2018
Habari ID: 3471577
TEHRAN (IQNA)- Kiongozi wa harakati ya mapambano ya Kiislamu ya Hizbullah ya Lebanon ameipongeza Malaysia kwa kuondoa askari wake katika muungano wa kijeshi unoongozwa na Saudia ambao umekuwa ukiwashambulia wananchi wasio na ulinzi Yemen tokea mwaka 2015.

Akihutubu kwa njia ya televisheni jana Ijumaa, Katibu Mkuu wa Hizbullah Sayyed Hassan Nasrallah alimpongeza Waziri Mkuu wa Malaysia Mahathir Mohammad kwa uamuzi wake wa kujiondoa katika muungano vamizi unaaongozwa na Saudia ambao umepelekea zaidi ya Wayemen 14,000 kupoteza maisha hadi sasa. Aghalabu ya walipoteza maisha ni raia wasio na hatia hasa wanawake na watoto.

Aidha amesema muungano huo unaoongozwa na Saudia pamoja na Imarati, kwa ushurukiano wa madola ya nchi za Magharibi, umepata hasara kubwa mikononi mwa wapiganaji wa Yemen katika bandari ya Al Hudaydah.

Kwingineko katika hotuba yake, Sayyed Hassan Nasrallah amesema matukio yanayojiri katika eneo la Mashariki ya Kati yana manufaa kwa kambi ya muqawama na mapambano na kwamba makundi yanayobeba silaha huko Syria yamo katika hali ya kusambaratika.

Amesema japokuwa hali ya sasa Mashariki ya Kati ina manufaa kwa kambi ya mapambano lakini kuna watu wanaotumia matukio hayo vibaya na kuna udharura wa kukomeshwa jambo hilo.

Katibu Mkuu wa Hizbullah ameashiria kushindwa kwa makundi ya kigaidi huko Syria na kusema kuwa, vita vya Syria ni vita vya eneo zima la Mashariki ya Kati na mustakbali wake na hii leo kunaonekana ishara za kusambaratika makundi ya kigaidi huko kusini mwa Syria.

Vilevile ametoa wito kwa wakimbizi wa Syria kurejea nchini kwao kwa hiari na kwamba harakati ya Hizbullah iko tayari kutoa msaada kuhusu suala hilo.

Katibu Mkuu wa Hizbullah pia ameashiria mashambulizi ya anga yaliyofanywa dhidi ya makundi ya mapambano huko Iraq karibu na mpaka wa nchi hiyo na Syria na kusema: Mashambulizi hayo hayapasi kupita hivi hivi bila ya kujibiwa.

Kuhusu hatua ya Marekani na kujiondoa katika makubaliano ya nyuklia ya Iran maarufu kama Mpango Kamili wa Pamoja wa Utekelezwaji,JCPOA, Sayyid Hassan Nasrullah amesema: Kujiondoa kwa Marekani katika makubaliano hayo, vitisho na vikwazo dhidi ya Iran ni sehemu ya mpango wa Marekani uliopewa jina la "Makubaliano ya Karne" ambayo lengo lake kuu ni kusambaratisha jitihada za Wapalestina kupata ukombozi.  

3466185

captcha