IQNA

Magaidi watekeleza mauaji wakati wa Sala ya Ijumaa msikitini Afghanistan,Marekani yalaumiwa

17:03 - August 04, 2018
Habari ID: 3471619
TEHRAN (IQNA)- Magaidi wakufurishaji wameushambulia msikiti wakati wa Swala ya Ijumaa katika mkoa wa Paktia mashariki mwa Afghanistan na kuua waumini wasiopungua 31 na kujeruhi wengine zaidi ya 80.

Walioshuhudia wanasema, wakati waumini walipokuwa wakiswali Swala ya Ijumaa magaidi waliingia ndani ya  Msikiti wa Imam Zaman (ATF) katika eneo la Khawaja Hassan mjini Gardez, ambapo walifyatua risasi na kujilipua miongoni mwa waumini waliokuwa wakiswali.

Rais Ashraf Ghani wa Afghanistan ametoa taarifa akilaani hujuma hiyo dhidi ya Msikiti wa Khawaja Hassan na kusema, mashambulizi kama hayo ya kigaidi hayawezi kufanikiwa kuvuruga umoja wa Waafghani.

Katika taarifa, Bahram Qassemi, msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran ametangaza mfungamano wa Iran na watu na serikali ya Afghanistan hasa familia za waathirika wa hujuma hiyo ya kigaidi na kusema: "Ugaidi ulioingiziwa kutoka nje na kulazimishwa kwa watu wa Afghanistan unalenga kuibua mifarakano kwa kuvuruga usalama katika taifa hilo." Hivyo ametoa wito kwa serikali ya Afghanistan  kuwa angalifu na itumie busara katika kuvunja njama hii na waliotenda jinai hiyo isiyo na mipaka wawajibishwe.

Baada ya hujuma hiyo, kundi la Taliban lilitoa taarifa na kusema halijahusika. Kundi la kigaidi la ISIS au Daesh ndilo ambalo kawaida hutangaza kuhusika na hujuma dhidi ya misikiti nchini Afghanistan.

Naye Zamir Kabulov, mjumbe maalumu wa rais wa Russia katika masuala ya Afghanistan hivi karibuni alitangaza kuwa kuna ushahidi unaoonyesha kwamba Marekani ikishirikiana na muungano wa kijeshi wa NATO inahusika katika kuwaingiza magaidi wa ISIS nchini Afghanistan kutoka Syria na Iraq.

Viongozi na wananchi wa Afghansitan pia wamebainisha wazi kuwa Marekani inaunga mkono kuenea kundi la ISIS nchini humo.

3466468

captcha