IQNA

19:18 - December 22, 2018
News ID: 3471782
TEHRAN (IQNA)- Sheikhe Mkuu wa Chuo cha Kiislamu cha Al Azhar nchini Misri, Sheikh Ahmed al-Tayeb amemtumia salamu za Krismasi, Papa Francis, Kiongozi wa Kanisa Katoliki duniani.

Kwa mujibu wa taarifa ya Al Azhar, Sheikh Tayyib alimpigia simu Papa Francis Jumanne 18, Disemba na awali akampongeza kwa munasaba wa siku yake ya kuzaliwa iliyokuwa 17 Disemba huku akimtakia amani na upendo.

Taarifa ya Al Azhar imeongeza kuwa, Sheikh Mkuu wa Al Azhar pia alimpa Papa Francis na Wakristo kote duniani salamu za pongezi, kwa munasaba wa kumbukumbu ya uzawa wa Nabi Isa Masih AS (Yesu) tarehe 25 Disemba, siku ambayo ni maarufu kama Krismasi.

Papa Francis alimshukuru Sheikh Tayyib kwa hatua yake nzuri yana kusema anasubiri kwa hamu kukutana naye hivi karibuni mjini Abu Dhabi katika Umoja wa Falme za Kiarabu. Mkutano wa kimataifa wa viongozi wa dini mbali mbali umepangwa kufanyika Abu Dhabi mnamo Februari 2019.

Mwaka 2017, Sheikh Tayyib alikutana na Papa Francis katika makao makuu ya Kanisa Katoliki Duniani, Vatican, ambapo walijadili jitihada za pamoja na kuleta amani na maelewano duniani.

Hivi karibuni pia, Taasisi ya Dar al-Ifta ya Misri ilitangaza inajuzu au inafaa kwa Waislamu kuwapongeza wasiokuwa Waislamu kwa munasaba wa siku kuu zao na kwamba hilo ni kwa mujibu wa mafundisho ya dini tukufu ya Kiislamu.

Dar al-Ifta ya Misri, inayoshughulikia masuala ya fatuwa za Kiislamu, imetangaza kuwa: "Mafundisho ya dini ya Kiislamu yanawahimiza Waislamu kutoa salamu za pongezi kwa wasiokuwa Waislamu katika idi na minasaba yao ya kidini na hili ni kwa mujibu wa ubora wa tabia njema ambazo alikuja nazo Mtume SAW."

Katika ujumbe wake wa video, Dar al-Ifta ya Misri imetoa wito kwa Waislamu kufuatia Sira ya Mtume Muhammad SAW na kuwataka wasitumbukie katika mitego ya makundi ya wenye misimamo mikali ya kufurutu ada ambao wanawakufurisha wale wote wasioafiki fikra zao finyu.

3773549

Name:
Email:
* Comment: