IQNA

Magaidi wa Al Shabab wahujumu hoteli ya kifahari Nairobi na kuua watu 21

20:43 - January 16, 2019
Habari ID: 3471808
TEHRAN (IQNA)- Magaidi wakufurishaji wa kundi la Al Shabab Jumanne walihujumu hoteli ya kifahari mjini Nairobi, Kenya na kuua watu 21.

 

Magaidi hao waliingia ndani ya hoteli ya Dusit Jumanne alasiri na oparesheni ya kuwatimua iliendelea hadi Jumatano alfajiri.

Akihutubia waandishi habari baada ya oparesheni hiyo kukamilika Rais Uhuru Kenyatta wa Kenya alisema magaidi wote wameuawa huku zaidi ya watu 700 wakiokolewa katika tukio hilo.

Kwenye picha za camera ya CCTV, washukiwa wanne wa kigaidi walionekana wakiingia kwenye jengo la hoteli ya kifahari ya Dusit ambayo ina ofisi, hoteli pamoja na benki na kuanza kushambulia watu kwa kuwapiga risasi. Rais Uhuru Kenyatta amepongeza vikosi vya usalama kwa kuwakabili magaidi hao.

Kwa mujibu wa maofisa wa usalama kulikuwa na magaidi watano waliouawa na vyombo vya usalama huku mmoja akijilipua.

Duru zinasema kuwa raia wa Uingereza na Mmarekani ni miongoni mwa watu waliouawa. Wakati huo huo, Marekani na Umoja wa Mataifa zimelaani kitendo hicho. Msemaji wa idara ya Ulinzi wa Marekani amekitaja kitendo hicho cha uvamizi kuwa cha kipumbavu huku katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres akikitaja kuwa uvamizi mbaya wa kigaidi.

Kundi la kigaidi na kitakfiri la al-Shabaab lenye makao yake nchini Somalia limetangaza kupitia radio yake ya kipropaganda ya Andalus kuwa limehusika na shambulizi hilo.

Msemaji wa genge hilo la ukufurishaji, Abdiasis Abu Musab amesema "Sisi ndio tumehusika na shambulizi la Nairobi. Operesheni inaendelea. Tutatoa maelezo zaidi baadaye."

Shambulizi hilo limetokea mita chache kutoka Jengo la Westgate ambalo lilishambuliwa na wanachama wa al-Shabaab mwaka 2013, ambapo watu 67 waliuawa.

3467713

captcha