IQNA

Hujuma za kigaidi zajiri Nigeria kabla ya kuanza uchaguzi mkuu

11:30 - February 23, 2019
Habari ID: 3471850
TEHRAN (IQNA)- Magaidi wakufurishaji wa Boko Haram mapema leo wameshambulia mji katika eneo la kaskazini mashariki mwa Nigeria na kuwalazimu wakazi kutoroka masaa machache tu kabla ya kuanza upigaji kura katika uchaguzi mkuu.

Taarifa zinasema hujuma hiyo imejiri katika mji wa Geidam jimboni Yobe na kupelekea mamia ya watu, wakiwemo wanawake na watoto kutoroka. Wakati wa hujuma hiyo mjini Geidam, pia kumesikika milipuko huko Maiduguri, mji mkuu wa jimbo jirani la Borno ambalo ni ngome ya magaidi wakufurishaji wa Boko Haram.

Hayo yanajiri huku uchaguzi mkuu ulioahirishwa kwa wiki moja nchini Nigeria, ukiwa unafanyika leo Jumamosi. Kuna wasiwasi kuwa idadi kubwa ya watu wanaona kwamba kujitokeza kwao vituoni ni kujiweka kwenye hatari ya kushambuliwa na kundi la Boko Haram.

Rais Muhammadu Buhari amewataka wananchi wa Nigeria wajitokeze kwenda kupiga kura na ameahidi kwamba utakuwepo usalama wa kutosha. Wagombea wawili wakuu ni rais Muhammadu Buhari, 76, na naibu wa rais wa zamani Atiku Abubakar, 72.

Tume huru ya uchaguzi nchini Nigeria wiki iliyopita iliahirisha uchaguzi huo wakati Wanigeria zaidi ya milioni 72 walipokuwa wanajitayarisha kwenda kupiga kura.

Akilihutubia taifa kwenye televisheni Rais Buhari amewataka Wanigeria wasiwe na wasiwasi na wawe na imani kwamba tume ya uchaguzi itatimiza jukumu lake. Naye mshindani wake kiongozi wa chama kikuu cha upinzani PDP Atiku Abubakar ametoa wito huo huo kwa wapiga kura.

Chama tawala cha All Progressives Congress (APC) kimeahidi kuipeleka nchi katika "hatua nyingine", akisema kuwa miaka minne ya kwanza ya utawala wa Buhari ulikuwa wa "kuunda mfumo wa kazi" japo matokeo ya kazi hiyo huenda hayakuonekana.

Abubakar na chama chake cha People's Democratic Party wameahidi "kuiwezesha Nigeria kufanya kazi tena", wakiongeza kuwa rais amewapotezea miaka minne.

Wote wawili wanatokea eneo la Kaskazini ambalo wakazi wake wengi ni Waislamu.

Zaidi ya Wanigeria milioni 84 wameandikishwa kupiga kura kwenye taifa hilo lenye wakaazi milioni 190 la magharibi mwa Afrika. Lakini kwenye maeneo mengi ya kaskazini, ambako uasi wa kundi la Boko Haram umesababisha vifo vya zaidi ya watu 27,000 na kuwafanya mamilioni kuyakimbia makazi yao yamkini idadi kubwa ya wapiga kura wasiweze kutekeleza haki yao ya kupiga kura.

3467977

captcha