IQNA

Uingereza yatakiwa kuwalinda Waislamu baada ya hujuma New Zealand

20:34 - March 20, 2019
Habari ID: 3471882
TEHRAN (IQNA)-Serikali ya Uingereza imetakiwa kuwapa Waislamu ulinzi kufuatia hujuma za Ijumaa iliyopita dhidi ya misikiti miwili nchini New Zealand.

Tume ya Kiislamu ya Haki za Binadamu (IHRC) yenye makao yake London, imemuandikia barua Waziri wa Mambo ya Ndani wa Uingereza Sajid Javid ikitaka Waislamu na wafuasi wa dini zingine za wachache wapewe ulinzi baada ya hujuma ya kigaidi kulenga Waislamu waliokuwa wakiswali Sala ya Ijumaa katika misikiti miwili mjini Christchurch nchini New Zealand. Hujuma hiyo ya kinyama ilipelekea Waislamu 50 kuuawa shahidi katika tukio ambalo limelaaniwa kote duniani.

Waislamu wengine karibu 50 wamejeruhiwa vibaya katika hujuma hiyo ambayo ilitekelezwa na gaidi raia wa Australia mwenye misimamo mikali ya ubaguzi, Brenton Tarrant, ambaye ni mfuasi sugu wa Rais Donald Trump wa Marekani aliye maarufu kwa misimamo yake dhidi ya Uislamu. Baada ya kugaidi huyo kutekeleza mauaji ya watu 42 katika msikiti wa Al Noor alielekea katika msikiti wa Linwood katika mji huo huo na kuua watu wengine 8.

IHRC imesema Waislamu Uingereza wanaendelea kukabiliwa na hatari na wanaishi katika mazingira ya hofu, hasa baada ya hujuma  ya mwaka 2017 iliyotekelezwa na gaidi Darren Osborne katika Msikiti wa Finsbury Park, mjini London. Katika hujuma hiyo Mohammad Saleem aliyekuwa na umri wa miaka 82 alidungwa kisu na kuuawa na gaidi huyo ambaye ni mfuasi wa makundi ya wazungu wabaguzi wenye misimamo mikali ya mrengo wa kushoto.

Ripoti ya IHRC imesema uchunguzi uliochapishwa mwaka 2015 umebaini kuwa asilimia 66 ya Waislamu Uingereza waliripoti kuongzeka vitendo vya chuki dhidi ya Waislamu katika hali ambayo mwaka 2010 kiwango hicho kilikuwa ni asilimia 39.8.

Serikali ya Uingereza inalaumiwa kwa kutochukua hatua zinazofaa kuwalinda Waislamu katika hali ambayo huchukua hatua za haraka kila kunapodaiwa kuwa ni chuki dhidi ya Mayahudi, sera ambayo imetajwa kuwa ni ubaguzi wa wazi.

/3468167

captcha