IQNA

Waziri Mkuu wa New Zealand aagiza uchunguzi huru kuhusu mauaji msikitini

12:08 - March 26, 2019
Habari ID: 3471888
TEHRAN (IQNA)- Waziri Mkuu wa New Zealand Jacind Ardern ameagiza kufanyike uchunguzi huru kuhusu hujuma za kigaidi dhidi ya misikiti miwili katika mji wa Christchurch nchini humo.

Bi. Ardern anataka uchunguzi huo ubaini kuwa iwapo kulikuwa na uzembe katika idara ya kiintelijinesia na polisi na hivyo kusababisha jinai hiyo.

"Wakati Wanezeland na Waislamu kote duniani wanaomboleza na kuliwazana, wana haki ya kuuliza ni vipi hujuma kama hii ya kigaidi imetokea hapa," amesema Ardern.

Akizungumza na waandishi habari Jumatatu katika Jengo la Bunge katika mji mkuu, Wellington, Bi. Adern amesema serikali yake itachukua hatua zote inazoweza katika uchunguzi kubaini iwapo kulikuwa na fursa la kuzuia uovu huo.

Wakati huo huo Idadi kubwa ya raia wa New Zealand wametaka Waziri Mkuu wa nchi hiyo, Jacinda Ardern atunukiwe tuzo ya amani ya Nobel kutokana na namna alivyoamiliana kwa njia bora na Waislamu baada ya shambulizi la kigaidi la hivi karibuni ndanii ya misikiti.

Kwa mujibu wa raia hao, miamala ya kuvutia iliyofanywa na waziri mkuu huyo baada ya hujuma hiyo ya kinyama dhidi ya Waislamu, ilikuwa ya kuigwa kutokana na upendo aliouonyesha kwa jamii ya Waislamu wa New Zealand. Hii ni kwa kuwa siku moja baada ya shambulio la kigaidi la tarehe 15 mwezi huu katika misikiti miwili ya mji wa Christchurch, sambamba na kufika eneo la tukio akiwa amevaa mtandio kichwani na kukutana pia na wawakilishi wa Kiislamu na kutoa pole kwa kuwakumbatia wanawake Waislamu kutokana na hujuma hiyo, alilaani vikali jinai hiyo ya kigaidi.

Aidha alisema kuwa, mateso wanayoyapata majeruhi wa hujuma hiyo ya kigaidi ni mateso ya taifa zima la New Zealand. Aidha Bi.Ardern aliwataka raia wote wa nchi hiyo pamoja na dunia nzima kuwaunga mkono wahanga wa shambulizi hilo la kinyama.

Katika fremu hiyo Ijumaa iliyopita, kulifanyika marasimu ya kuwaenzi wahanga wa hujuma hiyo katika uwanja wa mapumziko ulioko kando na msikiti wa al-Noor katika mji wa Christchurch ambapo maelfu ya raia wa New Zealand walifika eneo hilo wakiwa na mabango au vipeperushi vyenye kutoa alama ya upendo wao kwa jamii ya Waislamu wa nchi hiyo. Ijumaa iliyopita Bi. Adern aliamuru adhana irushwe hewani katika televisheni na radio ya kitaifa wakati wa Sala ya Ijumaa ili kuoneysha mshikamani na Waislamu.

Mbali na hayo mwanzoni mwa wiki jana, bunge la nchi hiyo lilifunguliwa kwa kisomo cha Qur'an Tukufu kama ishara ya kuonyesha mshikamano na Waislamu.

3468188

captcha