IQNA

Maadhimisho ya mwaka wa 43 wa Siku ya Ardhi Palestina

21:21 - March 31, 2019
Habari ID: 3471895
TEHRAN (IQNA)- Jumamosi tarehe 30 Machi 2019, imesadifiana na kuwadia mwaka wa 43 wa Siku ya Ardhi huko Palestina inayokaliwa kwa mabavu na utawala vamizi wa Israel.

Tarehe 30 Machi nayo ni miongoni mwa siku ambazo zina umuhimu wa aina yake katika kalenda na historia ya Palestina. Kwa hakika maadhimisho ya mwaka wa 43 wa Siku ya Ardhi yana umuhimu wa pande kadhaa kwa wananchi madhulumu wa Palestina.

Upande wa kwanza wa umuhimu wa siku hii ni wa kimaanawi. Tarehe 30 Machi 1976 viongozi wa utawala haramu wa Israel walipora maelfu ya hekari za ardhi za Wapalestina katika mji wa al-Khalil ulioko kaskazini mwa Palestina. Kufuatia hatua hiyo ya kijinai, wananchi wa Palestina walianzisha mgomo wa chakula na kufanya maandamano makubwa. Maandamano hayo ya Wapalestina ya kulalamikia hatua hiyo ya Israel ya kughusubu na kupora ardhi za wananchi hao madhulumu ilipelekea kutokea mapigano makali baina yao na wanajeshi wa utawala vamizi wa Israel. Wapalestina sita waliuawa shahidi kwa kupigwa risasi na maelfu ya wengine walijeruhiwa katika ghasia na sokomoko hilo.

Kwa muktadha huo, wananchi wa Palestina wa Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan na Ukanda wa Gaza na hata walioko katika kambi za wakimbizi huandamana kila mwaka katika siku kama ya leo kwa minajili ya kuwaenzi mashahidi wa mwaka 1976 na wakati huo huo kuonyesha upinzani wao dhidi ya utawala ghasibu wa Israel.

Upande wa pili wa umuhimu wa maadhimisho ya mwaka wa 43 wa Siku ya Ardhi ni wa kijiografia. Kama inavyoeleweka wazi kupitia jina la siku hii, maandamano haya ni sisitizo la wananchi wa Palestina la kulinda na kutetea ardhi zao zote na kusimama kidete mkabala na ukaliaji mabavu wa ardhi zao unaofanywa na utawala vamizi wa Israel. Katika kiipindi cha miaka ya hivi karibuni upande huu wa kijiografia umepata umuhimu maradufu, kwani Rais Donald Trump wa Marekani aliipatia rasmi Israel mji wa Beitul Muqaddas ambao kimsingi ni eneo lisilotenganishika kijiografia na kiutamabulisho wa kidini na Wapalestina.

Katika uwanja huu, maandamano ya mwaka jana ya Wapalestina ya Siku ya Ardhi yalikuwa na mahudhurio makubwa na utawala ghasibu wa Israel ulitenda jinai kubwa zaidi ya ile ya mwaka 1976. Katika maandamano ya mwaka 1976 wanajeshi wa Israel waliwauawa shahidi Wapalestina 6, lakini katika maandamano ya mwaka jana ya Siku ya Ardhi Wapalestina 18 waliuawa shahidi na wengine 1500 kujeruhiwa. 

Upande wa tatu wa umuhimu wa maandamano ya maadhimisho ya Siku ya Ardhi mwaka huu ni kusadifiana siku hii na maadhimisho ya mwaka wa kwanza wa maandamano ya 'Haki ya Kurejea. Maandamano ya ' Haki ya Kurejea" yalianza 30 Machi 2018 kwa shabaha ya kutetea ardhi zote za Palestina na kurejea wakimbizi wa Kipalestina katika ardhi za mababu zao. Katika kipindi cha mwaka mmoja uliopita, Wapalestina wamefanya maandamano hayo kwa wiki 52 mtawalia. Aidha katika kipindi cha mwaka mmoja uliopita, takribani Wapalestina 260 wameuawa shahidi katika maandamano ya Haki ya Kurejea na wengine zaidi ya 27,000 wamejeruhiwa.

Abu Hamza, msemaji wa Brigedi ya Quds, tawi la kijeshi la Harakati ya Jihadul Islami ya Palestina anabainisha moja ya mambo muhimu ya maadhimisho ya Siku ya Ardhi mwaka huu akisema: Maandamano ya kuunga mkono haki ya kurejea wakimbizi wa Kipalestina ambayo yameingia mwaka wake wa pili umuhimu wake kwa taifa letu si mdogo ikilinganishwa na maandamano ya Siku ya Ardhi.Maadhimisho ya mwaka wa 43 wa Siku ya Ardhi Palestina

Upande wa nne wa umuhimu wa maandamano ya Siku ya Ardhi mwaka huu unahusiana na kudhihirika wazi zaidi na bayana usuhuba na mapatano ya baadhi ya nchi za Kiarabu na utawala ghasibu wa Israel. Katika kipindi cha mwaka mmoja uliopita, mwenendo wa baadhi ya nchi za Kiarabu wa kutaka kuwa na uhusiano wa kawaida na utawala haramu wa Israel umedhihirika wazi zaidi, jambo ambalo ni sehemu ya mpango wa Marekani wa 'Muamala wa Karne'. 

Kwa msingi huo, maandamano ya leo ya Siku ya Ardhi ya Wapalestina yamesisitiza tena juu ya kuendelezwa muqawama na mapambano dhidi ya Israel na wakati huo huo kupinga mipango ya baadhi ya nchi za Kiarabu na harakati zao za kutaka kuwa na uhusiano wa kawaida na Israel. Aidha maandamano ya leo yametangaza kupinga kinagaubaga mpango wa Marekani uliojaa njama wa 'Muamala wa Karne'.

Nukta ya mwisho ni hii kwamba, matukio ya siku zenye nembo za Wapalestina huuweka pabaya utawala haramu wa Israel na kuufanya ukabiliwe na hali ngumu ikilinganishwa na siku nyingine. Hii ni kutokana na kuwa, siku hizi ikiwemo Siku ya Ardhi kwa mara nyingine tena hudhihirisha umuhimu wa kadhia ya Palestina kwa ulimwengu wa Kiislamu na wakati huo huo kuonyesha ukubwa wa jinai za utawala haramu wa Israel mbele ya fikra za waliowengi ulimwenguni.

/3800398

captcha