IQNA

Waislamu Ethiopia wanufaika na huduma za Kiislamu katika benki

14:30 - April 06, 2019
Habari ID: 3471901
TEHRAN (IQNA)- Waislamu nchini Ethiopia wanaendelea kunufaika na huduma za Kiislamu katika taasisi za kifedha nchini humo.

Shirika la kwanza kutoa huduma za kifedha kwa mujibu wa sheria za Kiislamu Ethiopia lilikuwa ni Somali Microfinance Institution (SMFI).

Kinyume na benki au mashirika mengine ya kifedha, mashirika ya kifedha ya Kiislamu huwa hayatozi riba kwa mikopo na pia hujizuia kuwekeza fedha za wateja katika sekta au huduma ambazo ni haramu kwa mujibu wa mafundisho ya Kiislamu kama vile pombe, kamari, uuzaji nyama ya nguruwe nk.

Changamoto kubwa ni kuwa Ethiopia bado iko nyuma katika kuwawezesha raia kutumia huduma za benki. Takwimu za Benki ya Dunia zinaonyesha kuwa idadi ya watu wazima wenye akaunti ya benki iliongezeka kutoka asilimia 22 mwaka 2014 hadi asilimia 35 mwaka 2017. Hii ni katika hali ambayo  katika nchi jirani ya Kenya, mwaka 2017 watu wazima waliokuwa na akaunti za benki mwaka  2017 walikuwa ni asilimia 82. Katika hali ambayo Waislamu ni karibu asilimia 35 ya watu wote milioni 105 nchini humo, taratibu za kuanzisha mfumo wa kifedha wa Kiislamu zilitangazwa na Benki ya Kitaifa ya Ethiopia (NBE) mwaka 2011, mwaka ambao SMFI ilianza shughuli zake.

SMFI imeweza kutoa huduma kwa wateja 30,000, aghalabu katika maeneo ya vijijini ya eneo la mashariki mwa Ethiopia ambalo wakaazi wake wengi ni wa asili ya Kisomali. SMFI inatazamia kuwa benki kamili ya Kiislamu na hivyo inatazamiwa kuwa benki ya kwanza ya aina hiyo nchni Ethiopia.

Benki hiyo ambayo itajulikana kama Zamzam Islamic Bank ilitarajiwa kuanzishwa mwaka 2012 lakini haikuweza kutimiza vigezo vya NBE.

Jitihada za kuandaa mazingira mazuri ya benki za Kiislamu Ethiopia zilishika kasi Aprili 2018 wakati alipoingia madarakani Waziri Mkuu Abiy Ahmed, Mkristo, ambaye baba yake ni Mwislamu.

Wengi wanazitazama benki za Kiislamu kama sehemu ya uwazi wa kiuchumi wenye lengo la kuwavutia wawekezaji nchini Ethiopia hasa kwa kuzingatia ukuraba wa nchi hiyo na eneo la Mashariki ya Kati (Asia Magharibi).

3468221

captcha