IQNA

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu

Marekani haitafika popote katika ukhabithi wake dhidi ya Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu

20:21 - April 09, 2019
Habari ID: 3471906
TEHRAN (IQNA)- Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema Marekani inahasimiana na Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu (IRGC) kwa sababu jeshi hilo limekuwa mstari wa mbele katika kuilinda Iran na Mapinduzi ya Kiislamu na kuongeza kuwa: "Kwa miaka 40 sasa, Marekani na maadui wengine wajinga wamekuwa wakifanya kila wawezalo dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran lakini wameshindwa."

Ayatullah Sayyed Ali Khamenei ameyasema hayo Jumatatu usiku mjini Tehran kwa munasaba wa Maulid ya Kiongozi wa Mashahidi, Imam Hussein AS ambayo pia huadhimishwa kama siku  ya Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu. Katika mkutano wake huo na baadhi ya familia za  askari wa IRGC, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amelitaja Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu kuwa taasisi muhimu ambayo iko mstari wa mbele katika kukabiliana na maadui katika medani mbali mbali. Ameongeza kuwa, IRGC imeweza kufika maelfu ya kilomita nje ya nchi katika oparesheni dhidi ya maadui mfano ukiwa ni kuongoza mapambano katika Haram ya Bibi Zainab SA na pia katika medani za kukabiliana kisiasa na adui.

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema nukta hizo ndio chanzo cha chuki za Marekani kwa IRGC. Ameongeza kuwa: "Marekani inadhani inaibua matatizo dhidi ya  IRGC, Mapinduzi ya Kiislamu na Iran lakini ukhabithi wao hautafika popote bali hila na njama zao zitawageukia na kuwadhuru wao wenyewe. Maadui wa Jamhuri ya Kiislamu kama vile Trump na wajinga wengine katika utawala wa Marekani wanaelekea kuangamia."

Kiongozi Muadhamu ameendelea kubaini kuwa, katika kipindi cha miaka 40 sasa maadui wamekuwa wakitekeleza njama dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran lakini pamoja na hayo Mapinduzi yameendelea kustawi na hilo linaashiria kushindwa Marekani katika kuzuia harakati za taifa la Iran. Ayatullah Khamenei amesema: "Katika kipindi cha miaka 40, Irani azizi imekabiliana na kila aina ya mashinikizo ya kisiasa, kiuchumi na kipropaganda lakini hata katika zama za awali za uhai wa Jamhuri ya Kiislamu, maadui hawakuweza kufanya chochote."

Ayatullah Khamenei ameashiria namna Jamhuri ya Kiislamu ya Iran inavyoongoza katika eneo na kusema: "Kinyume cha anavyodhania adui, izza na nguvu za leo za mfumo wa Kiislamu hazitokani na bomu la atomiki kwani kutoka awali Iran imesisitiza kuwa haihitajii silaha za nyuklia kwa sababu zinakinzana na mafundisho yetu ya kidini. Kwa hivyo nguvu na izza ya taifa la Iran leo kwa mtazamo wa ulimwengu wa Kiislamu inatokana na kusimama kidete, kujitolea muhanga na muono wa mbali wa wananchi."

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema ili harakati hii  iliyojaa fahari iweze kuendelea, kuna ulazima wa kutambua majukumu na kuyatekeleza.

Amebaini kuwa, bila shaka, Mapinduzi ya Kiislamu yatasonga mbele lakini pamoja na hayo wananchi wote, hasa vijana, Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu, vikosi vyote vya kijeshi na taasisi za serikali, wote kwa pamoja wanapaswa kutekeleza majukumu yao katika harakati hii na kuchukua kigezo katika vitendo vya waumini na Mawalii wa Mwenyezi Mungu na Imam Khomeini MA na pia watekeleze wajibu wao kwa ajili ya Mwenyezi Mungu na katika njia ya Mwenyezi Mungu.

Siku ya Jumatatu, mtawala wa Marekani Donald Trump alitoa taarifa na kusema analiweka Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu katika orodha ya Marekani ya makundi ya kigaidi, tangazo ambalo limeibua ghadhabu kubwa katika taifa la Iran na mataifa ya eneo.

3802273

captcha