IQNA

Utawala wa Israel walaaniwa duniani baada ya kubomoa nyumba za Wapalestina

12:59 - July 23, 2019
Habari ID: 3472054
TEHRAN (IQNA) -Jumuiya za kimataifa na taasisi kadhaa za kutetea haki za binadamu duniani zimelaani jinai iliyofanywa na utawala wa Kizayuni wa Israel ya kubomoa nyumba za Wapalestina kusini mwa Quds (Jerusalem) inayokaliwa kwa mabavu.

Hizbullah ya Lebanon imesema jinai hiyo ya utawala wa Kizayuni imetekelezwa kwa lengo la kuwahamisha kwa nguvu wananchi madhulumu wa Palestina.

Harakati hiyo ya muqawama imetoa taarifa ya kulaani hatua ya kuwahamisha kwa nguvu Wapalestina na kueleza kwamba: Hatua yoyote ya kuanzisha uhusiano wa kawaida na Israel itakayofifilisha kisiasa jinai za Wazayuni maghasibu bila shaka itafeli tu.

Shirika la kimataifa la kutetea haki za binadamu la Amnesty International limesema, badala ya kubomoa nyumba za Wapalestina, Israel ilipaswa kubomoa baadhi ya sehemu za ukuta wa uzio ulioko ndani ya ardhi za Palestina unazozikalia kwa mabavu, ambao wenyewe ni ukiukaji wa sheria za kimataifa. Shirika hilo la msamaha duniani limeitaka Jamii ya Kimataifa iwashinikize viongozi wa utawala haramu wa Israel kuhakikisha utawala huo ghasibu unatekeleza majukumu yake kulingana na sheria za haki za binadamu na kutoa hakikisho la kuwalinda Wapalestina wanaoishi katika ardhi unazozikalia kwa mabavu.

Umoja wa Ulaya umesema, sera za ujenzi wa vitongoji inayotekelezwa na Wazayuni inakiuka sheria na imeitaka Tel Aviv isimamishe ubomoaji wa nyumba za Wapalestina haraka iwezekanavyo.

Jumuiya ya Ushirikiano wa Kiislamu (OIC), Qatar, Jordan na makundi ya Kipalestina nayo pia yamelaani jinai hiyo ya utawala wa Kizayuni.

Jeshi la utawala dhalimu wa Israel, jana Jumatatu liliwatoa majumbani mwao kwa nguvu Wapalestina kadhaa na kubomoa makumi ya nyumba za Wapalestina hao katika eneo la Wadil-Hums kusini mwa mji wa Baitul Muqaddas unaokaliwa kwa mabavu na utawala huo ghasibu.

Utawala wa Kizayuni umepanga kubomoa nyumba nyingine zaidi ya 200 za Wapalestina katika mji huo wa Quds mnamo siku zijazo.

Utawala haramu wa Israel unabomoa nyumba za Wapalestina na kujenga mahala pake vitongoji vya walowezi wa Kizayuni kinyume na sheria za kimataifa.

Itakumbukwa kuwa tarehe 23 Desemba mwaka 2016, Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa lilipitisha azimio linalotaka kukomeshwa ujenzi wa vitongoji vya walowezi wa Kizayuni katika ardhi za Palestina zinazokaliwa kwa mabavu

3469019

captcha