IQNA

Inna Lillah wa Inna Ilayhi Rajioun

Mtarjumi maarufu wa Qur'ani kwa lugha ya Kifaransa afariki Kodivaa

13:14 - August 27, 2019
1
Habari ID: 3472103
TEHRAN (IQNA) – Yahya (Christian) Bonaud, mwanafikra Mfaransa, msomi na mtarjumi wa Qur'ani Tukufu kwa lugha ya Kifaransa amefariki Jumatatu akiwa na umri wa miaka 62.

Bonaud amefariki katika ajali ya barabarani akiwa safarini nchini Kodivaa (Ivory Coast) alikokuwa amefika kwa ajili ya kutoa mihadhara katika Mwezi wa Muharram kuhusu tukio la Ashura la kuuawa shahidi Imam Hussein AS.

Bonaud alizaliwa mwaka 1957 huko Freiburg Ujerumani katika familia asili ya Kifaransa ambayo ilikuwa inafungamana kikamilifu na itikadi za Kikatoliki. Aliishi Ujerumani na kisha Algeria hadi umri wa miaka 10 na baada ya hapo wakahamia katika mji wa Strasbourg kaskazini mashariki mwa Ufaransa.

Alivutiwa sana na dini za ulimwengu wa mashariki na akaanza kufanya utafiti kuhusu dini hizo huku akitembelea nchi kama vile Uhispania, Morocco, Italia, Uholanzi na Ubelgiki kwa ajili ya utafiti.

Alichungza kwa kina maandishi ya mwanafalsafa Muislamu Mfaransa René-Jean-Marie-Joseph Guénon, ambaye pia ni maarufu kama ʿAbd al-Wāḥid Yaḥyá, na kutokana na taathira ya vitabu vya mwanafalsafa huyo hatimaye aliukubali Uislamu maishani mwaka 1979 na kubadilisha jina lake kuwa, Yahya.

Bonaud alipata shahada yake ya Uzamivu (Phd) kutoka Chuo Kikuu cha Sorbonne cha Ufaransa mwaka 1995. Tasnifu yake ya shahada ya uzamivu ambayo ilikuwa na anwani ya  "Thiolojia ya Maandishi ya Kifalsafa na Maarifa ya Kumjua Mungu ya Imam Khomeini" iliteuliwa kuwa utafiti bora mwaka 1999.

Wakati akifanya utafiti kuhusu tasnifu yake, Bonaud alifika Iran na kusoma falsafa ya Kiislamu na Maarifa ya Kumjua Mungu chini ya usimamizi wa Sayyed Jalal Ashtiani huko Mashhad mji iliko Haram ya Imam Ridha AS. Bonaud aliishi Mashhad kwa muda wa miaka 13 na alivutiwa sana na fikra za Imam Ridha AS. Mwaka 2001 alitunukiwa hadhi ya Mtumishi wa Imam Ridha AS.

Katika miaka ya hivi karibuni alifanya utafiti wa kina kumhusu mwanafalsafa maarufu wa Iran Mulla Sadra. Bonaud pia alitayarisha tarjumi ya Qur'ani Tukufu kwa lugha ya Kifaransa inayoweza kueleweka na watu wa matabaka yote.

Tayari kuna tarjumi zaidi ya 30 za Qur'ani kwa lugha ya Kifaransa lakini zina makosa mengi kutokana na kuwa baadhi zimeandikwa na mustashrikin (orientalists) ambao si Waislamu na walikuwa na chuki zao wakati wa kuandika tarjumi zao za Qur'ani. Aidha baadhi ya tarjumi zimeandikwa na Waislamu ambao ufahamu wao wa Kifaransa ulikuwa dhaifu.

Kwa msingi huo, Bonaud, na Javad Hadidi, msomi wa Kiislamu ambaye ana Shahada ya Uzamivu ya Lugha ya Kifaransa walianza mradi wa kutayarisha tarjumi mpya ya Qur'ani kwa lugha ya Kifaransa ambayo haina makosa wala udhaifu wa tarjumi zingine. Mradi huo ulimalizika baada ya miaka mitatu ya juhudi za pamoja na tarjumi ya Qur'ani ambayo wamechapisha ni ya kurasa 624 na inajumuisha pia tafsiri ya sura za Fatiha na Baqara. Walishakikhsa kuwa katika tarjumi yao  hawakuathiriwa na tarjumi zilizotangulia bali walianza upya kazi yao na hivyo tarjumi yao imetajwa kuwa miongoni mwa bora tarjumi bora zaidi za Qur'ani Tukufu kwa lugha za Ulaya.

3837766

Imechapishwa: 1
Inatathminiwa: 0
Haiwezi kuchapishwa: 0
Bila jina
0
0
Innalilah wa inna ilayhi raji'una

Allah ayifanye kabli yake iwe nimiongoni mwa bustani za djanna amuweke Pamoja na Imam Hussein Sayed shohadaa Pamoja na Maswumina 14
captcha