IQNA

Jeshi la India lawakandamiza Waislamu wa madhehebu ya Shia

18:28 - September 08, 2019
Habari ID: 3472120
TEHRAN (IQNA) – India imeweka sheria ya kutotoka nje katika sehemu kadhaa la eneo linalozozaniwa la Kashmir baada ya jeshi kkuwashambulia Waislamu wa madhehebu ya Shia waliokuwa wanashiriki katika maombolezo ya mwezi wa Muharram.

Kwa mujibu wa taarifa karibu Waislamu 12 walijeruhiwa Ijumaa jioni wakati wanajeshi wa India walipojaribu kuzuia matembezi ya maombolezo ya mwezi wa Muharram.

Muharram ni mwezi wa kwanza katika kalenda ya Kiislamu ya Hijria Qamaria. Waislamu wa madhehebu ya Shia na wengine kote duniani hujumuika katika siku 10 za kwanza za Muharram kuomboleza kuuawa shahidi mjukuu wa Mtume Muhammad SAW, Imam Hussein AS pamoja na wafuasi wake watiifu.

Wakati huo huo, mwanachuoni mashuhuri hapa nchini Iran sambamba na kusisitiza kuwa Jamhuri ya Kiislamu itaendelea kuwaunga mkono Waislamu wanaodhulumiwa wa eneo la Kashmir, amewataka Wakashmir waendelee kusimama kidete na kudumisha moyo wa muqawama.

Ayatullah Hossein Noori-Hamedani mmoja wa marajii taqlidi wa Waislamu wa madhehebu ya Shia ametoa mwito huo leo Jumapili katika mji wa Qom, kusini mwa Tehran hapa nchini, katika mazungumzo yake na wanazuoni kadhaa wa eneo la Kashmir.

Ameeleza bayana kuwa, Waislamu wana jukumu la kuwa macho na kusimama kidete dhidi ya njama za maadui. Ayatullah Hossein Noori-Hamedani amefafanua kuwa, "India, Pakistan na Bangladesh zilikuwa eneo moja, lakini Waingereza waliliteganisha ili kuibua uhasama na mgawanyiko, na kusababisha hali ya sasa ya mpasuko katika eneo la Kashmir."

Msomi huyo wa Kiislamu hapa nchini ameongeza kuwa, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran haitachoka kuwasaidia na kuwaunga mkono wanaodhulumiwa, sanjari na kusimama kidete dhidi mabeberu.

Mwezi uliopita wa Agosti, Waziri Mkuu wa India Narendra Modi alibatilisha mamlaka ya kujitawala eneo la Kashmir hatua ambayo Pakistan iliitaja kuwa kinyume cha sheria.

Inafaa kuashiria hapa kuwa, sehemu moja ya Kashmir iko chini ya udhibiti wa India na nyingine iko Pakistan. Nchi zote mbili zinadai kuwa wamiliki wa Kashmir yote. Mgogoro wa Kashmir ulianza wakati Pakistan na India zilipotengana mwaka 1947 baada ya kuondoka mkoloni Muingereza ambaye alipanda mbegu za chuki baina ya mataifa hayo mawili.  Wakaazi wa eneo la Kashmir linalotawaliwa na India wanataka kura ya maoni iainishe hatima yao ya ima kubakia India, kupata uhuru kamili au kujiunga na Pakistan. India inapinga vikali pendekezo hilo la kura ya maoni ya kuamua hatima ya Kashmir, eneo ambalo wakaazi wake wengi ni Waislamu.

3469361/

captcha