IQNA

Nasrallah: Kuuawa Sheikh Nimr ni ishara ya kuangamia utawala wa kitakfiri Saudia

11:17 - January 04, 2016
Habari ID: 3470012
Katibu Mkuu Harakati ya Hizbullah ya Lebanon amesema hatua ya utawala wa Saudi Arabia kumuua kidhulma mwanazuoni wa Kiislamu Sheikh Nimr Baqir al Nimr ni ishara ya kuanza kuangamia utawala huo wa kifalme ufuatao misingi ya kuwakufurisha Waislamu.

Sayyed Hassan Nasrallah ameyasema hayo Jumapili mjini Beirut katika hotuba ya moja kwa moja kwa njia ya Televisheni Jumapili katika hafla ya kumkumbuka marhum Sheikh Mohammad Ali Khatoun, mwanachama mwandamizi wa harakati hiyo. Akiashiria jinai ya Saudi Arabia katika kumnyonga Sheikh Nimr, amesema haiwezekani kufumbia macho jinai hiyo ya kinyama dhidi ya mwanazuoni huyo wa ngazi za juu. Ameongeza kuwa Saudi Arabia ni mwanzilishi wa makundi ya magaidi wakufurishaji duniani. Aidha ameitaja kuwa jinai ya kuogofya hatua ya utawala wa Saudia Arabia kumuua shahidi mwanazuoni maarufu wa Kiislamu Saudia Sheikh Nimr.

Katibu Mkuu wa Harakati ya Hizbullah ya Lebanon ameashiria umuhimu na hadhi aliyokuwanayo Sheikh Nimr kwa umma wa Kiislamu na kusema kuwa, utawala wa Aal Saudi unadai kutetea demokrasia na uhuru katika eneo lakini unapinga kukosolewa huku ukiwakandamiza wale wanaotaka mabadiliko.

Sayyid Hassan Nasrallah amesema Sheikh Nimr daima alifuata mkondo wa amani kama maulamaa wengine wa mashariki mwa Saudia na Bahrain. Ameongeza kuwa vyombo vya mahakama vya Saudia vimemyonga Sheikh Nimr kutokana na ushujaa wa aina yake aliokuwa nao mwanazuoni huyo mkubwa na mwanamapambano. Amesema mahakama za utawala wa Saudia hazikuweza kuthibitisha madai yao dhidi ya mwanazuoni huyo.

Katibu Mkuu wa Hizbullah ya Lebanon ameongeza kuwa mahakama za Saudia zilitoa madai yasiyo na msingi dhidi ya Sheikh Nimr kuwa eti alikuwa na silaha na kwamba eti aliunda kundi lenye silaha kukabiliana utawala wa kifalme nchini humo na kusema kuwa, wakuu wa Saudia walihisi kuwa ushujaa na kauli ya haki ya mwanazuoni huyo ni tishio kwao.

Sayyid Nasrallah ameendelea kusema kuwa, kwa kuuawa shahidi na kidhulma, Sheikh Nimr amefuata mkondo na mitume na chuo cha Karbala. Kiongozi wa Hizbullah ametuma salamu zake za rambi rambi kwa familia ya Shahidi Sheikh Nimr, Waislamu na maulamaa wa Kiislamu kote duniani. Huku akilaani vikali jinai hiyo ya Saudia ya kumuua Sheikh Nimr, Sayyid Nasrallah amesema Saudi Arabia itafeli katika njama zake za kuvuruga harakati ya mapambano ya Kiislamu ya Hizbullah nchini Lebanon.

3464308


captcha