IQNA

Mauaji ya Sheikh Baqir al Nimr yaendelea kulaaniwa

9:11 - January 06, 2016
1
Habari ID: 3470020
Licha ya kupita siku tano sasa tangu utawala wa kizazi cha Aal Saud huko Saudi Arabia utekeleze hukumu ya kifo dhidi ya mwanazuoni mashuhuri wa nchi hiyo, Sheikh Nimr Baqir al Nimr, aliyekuwa maarufu kwa kukosoa dhulma na ukandamizaji wa dola, wimbi la laani na lawama za kimataifa linaendelea kurindima dhidi ya ukatili huo.

Jumamosi iliyopita serikali ya Saudia ilitangaza kuwa, imewanyonga watu 47 akiwemo mwanazuoni na mtetezi wa haki za binadamu Sheikh Baqir al Nimr ambaye alikuwa mwasisi wa kituo cha kidini cha eneo la al Awwamiyyah huko mashariki mwa nchi hiyo.

Sheikh Nimr ambaye alikamatwa na kutiwa jela muda mfupi baada ya kuanza harakati ya wananchi wa Saudi Arabia ya kupinga siasa za kibaguzi za utawala wa kizazi cha Aal Saud hapo mwaka 2011 kwa tuhuma za kuchochea wananchi na kuongoza harakati ya upinzani ya Waislamu wa madhehebu ya Shia, mwaka jana alihukumiwa kifo na mahakama ya nchi hiyo inayosimamiwa moja kwa moja na mfalme wa Saudia.

Kamishna Mkuu wa Haki za Binadamu wa Umoja wa Mataifa ametoa taarifa akiitaja hatua ya serikali ya Saudia ya kuwanyonga makumi ya raia akiwemo, Sheikh Nimr, kuwa si ya kisheria na kutangaza kuwa: Kunyongwa kwa watu ambao walinyimwa hata haki ya kuwa na wakili mahakamani na ambao pia hatia yao haijathibitishwa ni kitendo cha kihalifu na jinai na hakiwezi kukubalika. Zeid Ra'ad Al Hussein Kamishna Mkuu wa Haki za Binadamu wa Umoja wa Mataifa ameeleza wasiwasi wake kuhusu ongezeko lisilo na kifani la kesi za kunyongwa watu nchini Saudi Arabia na kusema: Riyadh haipasi kuwanyonga raia na wapinzani kwa sababu tu ya kutoa maoni yanayopinga serikali na utawala.

Waziri wa Mambo ya Nje wa Italia, Paolo Gentiloni ameeleza wasiwasi wake kuhusu kuuliwa mwanazuoni huyo wa Kiislamu wa Saudia na kusema, kuuliwa kwa Sheikh Nimr kutazidisha machafuko ya kimadhehebu katika eneo la Mashariki ya Kati.

Nalo gazeti la Guardian la Uingereza limesema kufuatia kuuliwa Sheikh Nimr kutashuhudiwa kuongezeka kutoridika wananchi ndani ya utawala wa Saudia.

Kwa upande wake Sheikh Khalif Al Malaa Mkuu wa Jumuiya ya Maulamaa wa Ahlu Sunna Iraq amesema Saudi Arabia imezidihsa migogoro ya kieneo kwak kumuua Sheikh Nimr.

Maafisa wa Wizara za Mashauri ya Kigeni za Ufaransa, Ujerumani na Uingereza ambao ni washirika wakubwa wa Saudia Arabia kutokana na kuiuzia nchi hiyo silaha za mabilioni ya dola, pia wamekosoa vikali kitendo cha kunyongwa mwanazuoni huyo wa Kiislamu na kutangaza kuwa, kitendo hicho kinautia wasiwasi Umoja wa Ulaya kuhusu uwezekano wa kuongezeka machafuko katika Mashariki ya Kati.

Kwa upande wake Zuhairi Masrawi mshauri wa vyombo vya habari wa Rais wa Indonesia, amekosoa mwenendo wa Saudia wa kutaka kuzidisha machafuko na kusema kuuliwa kwa Sheikh Baqir Nimr kwa sababu tu ya kupinga dhulma na ukandamizaji wa serikali ni kielelezo cha juhudi za serikali ya Riyadh za kutaka kuzima sauti za kupigania haki nchini humo.

Kiongozi Mkuu wa Waislamu wa madhehebu ya Shia nchini Iraq, Ayatullah Ali Sistani amelaani vikali kitendo cha kunyongwa Sheikh mpigania mageuzi Baqir Nimr na kusema, lengo la kitendo hicho ni kutaka kupotosha fikra za watu kuhusu jinai zinazofanywa na utawala wa kizazi cha Aal Saud katika maeneo mbalimbali ya Mashariki ya Kati.

Sambamba na hayo ripoti zinasema wimbi la malalamiko na maandamano ya kupinga kitendo cha Saudia cha kumuua shahidi Sheikh Baqir Nimr limeenea katika nchi mbalimbali kama Uturuki, Pakistan, India, Lebanon, Bahrain, Iraq na kadhalika. Waandamanaji hao wameitaka jamii ya kimataifa kukomesha jinai za Saudi Arabia katika nchi mbalimbali kama Yemen, Syria na kwengineko.

Ripoti kutoka Saudi Arabia kwenyewe zinasema wakazi wa maeneo ya Qatif na al Awwamiyyah huko mashariki mwa nchi hiyo jana Jumapili waliandamana mitaani na kumkumbuka Sheikh Baqir Nimr katika shughuli iliyofanana na kusindikiza jeneza. Itakumbuka kwamba serikali ya Saudia imekataa kukabidhi maiti ya mwanazuoni huyo kwa familia yake na imemzika mapala pasipojulikana.

Rais Hassan Rouhani wa Iran pia ametoa ujumbe akiitaja hatua ya Saudia ya kumuua shahidi Sheikh Nimr kuwa ni ya kichochezi na kusema, licha ya kwamba Waislamu wote duniani wanalaani vikali kitendi hicho lakini wananchi Waislamu wa Iran hawataruhusu hatua hiyo inayopingana na Uislamu kutumiwa kama kisingizio cha kufanya mambo yanayopingana na sheria na yanayovunjia heshima Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.

3464782&3464354

Imechapishwa: 1
Inatathminiwa: 0
Haiwezi kuchapishwa: 0
إبرهيم يوسوف
0
0
Iran na nchi zingine ziungane na wakomeshe ukatili huo jamani.
captcha