IQNA

Mwanachuoni wa Kisunni Lebanon

Maulamaa wafichue kuhusu ISIS wanavyopotosha Qur’ani

12:53 - January 20, 2016
Habari ID: 3470070
Mwanachuoni wa Ahlul Sunna nchini Lebanon ametaka maulamaa Waislamu kote duniani kufichua kuhusu namna kundi la magaidi wakufurishaji wa ISIS au Daesh wanavyopotosha Qur’ani Tukufu.

Sheikh Hessam Al Aylani ambaye pia ni Imamu wa msikiti wa Ghafran katika mji wa Seida kusini mwa Lebanon amesema: "Vinara wa kundi la ISIS wanafuatilia maslahi yao binafsi huku wakiwasilisha tafsiri potovu za baadhi ya aya za Qur’ani ili kwa njia hiyo kutetea jinai na ukatili wao.”

Amongeza kuwa ili kukabiliana na tafsiri potovu ya ISIS kuhusu baadhi ya aya za Qur’ani na ili kuzuia kuchafuliwa jina Uislamu, maulamaa Waislamu wana wajibu wa kubainisha tafsiri sahihi na ya pamoja ya aya za Qur’ani. Amesema hatua hiyo itapelekea wote wafahamu ukweli na hivyo vinara wa magaidi wa ISIS hawataweza kupotosha aya hizo takatifu.

Sheikh Aylani amesema maulamaa wa Ahlul Sunna wanapaswa kuchukua hatua zaidi kukabiliana na fikra potovu za magaidi wa ISIS na kuongeza kuwa, ‘ISIS si tishio kwa Mashia tu bali pia ni hatari zaidi kwa Masunni.’ Amesema ISIS wanawaua Masunni katika maeneo wanayoyashikilia. Ameseisitza kuwa magaidi wa ISIS hawana uhusiano wowote na Ahul Sunna na kwamba maadui wa Uislamu ndio wanaowanasibisha na Usunni.

Mwanachuoni huyo wa Lebanon pia ametoa wito kwa kuimarisha umoja wa Waislamu kote duniani ili kukabiliana na kundi la wakufurishaji wa ISIS.

3468882

captcha