Kwa mujibu wa mwandishi wa IQNA, ukosefu wa serikali ya kitaifa Libya
sambamba na kuwepo utajiri wa mafuta ni nukta ambazo zimepelekea vinara wa
kundi la kigaidi la ISIS kuelekea katika nchi hiyo ya Afrika Kaskazini.
Baada ya kuanguka utawala wa dikteta Gaddafi mwaka 2011, nchi hiyo
iligeuka na kuwa medani ya mapigano baina ya makundi mbali mbali ya wanamgambo
na makundi ya magaidi wakufurishaji nchini humo. Hivi sasa magaidi wa ISIS
wanadhibiti miji kadhaa ya pwani ya
Libya kama vile Sirte, Bin Jawad, na Derna.
Hivi karibuni iliripotiwa kuwa
magaidi 500 wa ISIS walionekana wakielekea Libya. Miezi miwili iliyopita
Umoja wa Mataifa ulichapisha ripoti iliyobaini kuwa kuna magaidi 3000
wanaoendesha oparesheni zao za kihalifu nchini Libya. Duru nchini Libya
zinataja idadi hiyo kuwa takribani 10,000.
Mwaka 2015, idadi kubwa ya
magaidi wa ISIS nchini Libya walijiunga
na kundi la wanamgmabo wanaojiita Ansar Sharia. Wanamgambo hao wametangaza
utiifu wao kwa ISIS. Katika wiki za hivi karibuni pia, makundi mengine mawili
yaani, "Baraza la Kimapinduzi la Ajdabiya" na kundi jingine la
wanamgmabo huko Misrata walitangaza kujiunga na ISIS.
Wakuu wa Libya wanasema magaidi wa ISIS wanalenga kuteka vituo vya uzalishaji
mafuta nchini humo. Siku chache zilizopita, vituo viwili vya kuuza mafuta ghafi
ya petroli ya Libya katika masoko ya kimataifa vya Es Sider na Ra's Lanuf
vilishambuliwa na magaidi wa ISIS.
Kundu la kigaidi la ISIS linalenga kudhibiti vituo vya mafuta Libya ili
kuweza kupata pato kama ilivyo huko Iraq na Libya. Kukosekana serikali yenye
nguvu Libya pamoja na mapigano ya ndani ni mambo ambayo yametoa mwanya kwa ISIS
kujipenyeza Libya. Imearifiwa kuwa magaidi wa ISIS wamekimbilia Libya baada ya
kupata pigo Syria na Iraq kufuatia mafanikio ya majeshi ya nchi hizo.
3469535