IQNA

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu

Mapinduzi yatafanikiwa kwa 'Jihadi Kubwa', yaani kutomtii adui.

10:39 - May 27, 2016
Habari ID: 3470340
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema njia pekee ya kuufanya Mfumo wa Kiislamu udumu na kupiga hatua mbele na kufikiwa malengo ya Mapinduzi ni 'nchi kuwa na uwezo halisi' na kutekelezwa 'jihadi kubwa', yaani kutomtii adui.

Ayatullah Sayyid Ali Khamenei, ameyasema hayo Alkhamisi mjini Tehran katika mkutano na Mkuu na wajumbe wa Baraza la Tano la Wanazuoni Wataalamu wa Kumchagua Kiongozi Mkuu, ambapo mbali na kubainisha utambulisho na njia ya kimapinduzi ya baraza hilo amesema, Baraza la Wanazuoni Wataalamu ni kitu chenye adhama ya kweli.

Sambamba na kusisitiza kwamba njia na malengo ya Baraza la Wanazuoni Wataalamu inapasa kuwa njia na malengo yale yale ya Mapinduzi, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amefafanua kwa kusema: "Kutawala Uislamu", "Uhuru", "Kujitawala", "Uadilifu wa Kijamii", "Ustawi wa Jamii", "Kutokomeza umasikini na Ujinga", "Kuwa na muqawma wa kukabiliana na wimbi hatari la ufisadi wa kiakhlaqi, kiuchumi, kijamii na kisiasa lililoko Magharibi" na "Kusimama imara katika kukabiliana na ubeberu wa kambi ya Uistikbari" ni miongoni mwa malengo muhimu zaidi ya Mapinduzi ya Kiislamu ya taifa la Iran.

Ayatullah Khamenei amekumbusha kuwa Uislamu, bila ya shaka yoyote ni mtokomezaji wa dhulma na Uistikbari, hata hivyo akasisitizia kwa kusema: Lakini Uislamu unaoweza kuwa na muqawama wa kuweza kusimama imara kukabiliana na wababe na watumiaji mabavu duniani na kuitokomeza kambi ya ubeberu ni ule Uislamu ulio katika sura ya mfumo wa utawala na wenye nyenzo za madaraka na nguvu za kijeshi, kisiasa, kiuchumi, kiutamaduni na za vyombo vya habari.

/3501306

captcha