IQNA

Magaidi wa ISIS wanatega mabomu ndani ya Nakala za Qur'ani ili kukwepa kushindwa Fallujah

13:39 - June 09, 2016
Habari ID: 3470373
Waziri wa Mashauri ya Kigeni Iraq, Ibrahim Jafari amesema magaidi wa ISIS (Daesh) wanatega mabomu ndani ya nakala za Qur'ani Tukufu ili kuzuia jeshi la Iraq kuingia mji wa Fallujah.

Kwa mujibu wa mwandishi wa IQNA, Jafari amesema mbinu zinazotumiwa na ISIS ni kinyume cha mafundisho ya Kiislamu.

Ameongeza kuwa vitendo kama hivyo vya ISIS vya kuivunjia heshima Qur'ani Tukufu vinaimarisha irada na azma ya jeshi la Iraq na wananchi waliojitolea kukabiliana na kundi hilo la kigaidi.

Operesheni ya kuukomboa mji wa Fallujah uliovamiwa na kukaliwa kwa mabavu na kundi la kigaidi na kitakfiri la ISIS ilianza tarehe 23 ya mwezi uliopita wa Mei kwa amri ya Waziri Mkuu wa Iraq Haidar al-Abadi.

Aidha amesema operesheni ya kijeshi katika mji wa Fallujah ulioko katika mkoa wa Al-Anbar magharibi mwa nchi hiyo itaendelea hadi kuhakikisha uvamizi wa kundi la kigaidi la ISISkatika mji huo unahatimishwa.

Amesitiza juu ya kuendelea bila ya kusita operesheni ya kuukomboa mji wa Fallujah, al-Abadi ameeleza pia kuwa vikosi vya Iraq vinaendelea kusonga mbele ndani ya mji huo.

Waziri Mkuu wa Iraq ameongeza kuwa vikosi vya jeshi na vya kujitolea vya wananchi vinaendelea kusonga mbele ndani ya mji wa Fallujah na vitaendelea kupambana na Madaesh sambamba na kuzingatia kulinda maisha na mali za raia wa Iraq.

Huku akisisitizia kulindwa na kudhibitiwa maeneo yaliyokombolewa kutoka kwenye uvamizi wa kundi la kigaidi na kitakfiri la Daesh, al-Abadi amebainisha kuwa magaidi wa Daesh hawana njia ya kukimbilia kwa sababu njia zao zote za kutorokea zimefungwa.

Waziri Mkuu wa Iraq ambaye pia ni kamanda mkuu wa vikosi vya ulinzi vya nchi hiyo amebainisha kwamba waungaji mkono wa magaidi wanaendesha harakati za kueneza taarifa za uongo katika baadhi ya mitandao ya satalaiti ya Kiarabu pamoja na baadhi ya kanali za Kiiraqi na akasisitiza kwa kusema, Iraq itafungua mashtaka dhidi yao katika duru za kimataifa.

3504992

captcha