IQNA

Hekima ya Imam Ridha AS katika kujadiliana

10:34 - August 14, 2016
Habari ID: 3470520
Tarehe 11 Mfunguo Pili Dhil Qaada ni siku ya maadhimisho ya kuzaliwa Imam Ali bin Musa ar-Ridha AS, mjukuu wa Mtume Mtukufu SAW.

Imam Ridha AS ni kiongozi ambaye kwa zaidi ya miaka 1000 iliyopita aliingia katika ardhi ya Iran na kufuatia ujio wake huo, wapenzi wa Mtume na Ahlu Bait wake AS wakajaa furaha na msisimko. Katika siku kama hii nyoyo zote zimeelekea katika haram ya Imam Ridha AS. Licha ya kupita karne nyingi lakini bado wapenzi na wafuasi wa mtukufu huyo kutoka pembe zote za dunia humiminika kwa wingi katika mji mtakatafu wa Mash'had ulioko kaskazini mashariki mwa Iran ili wapate kupitisha masaa na siku chache katika mji huo mtakatifu kwa madhumuni ya kukata kiu yao ya kimaanawi kwa kuzuru kaburi takatifu la mjukuu huyo wa Mtume SAW.
Wimbi hili kubwa la wapenzi wanaomzuru Imam Ridha AS linakumbusha zama ambazo Imam alitoka katika mji mtakatifu wa Madina kuelekea katika ardhi ya Marw nchini Iran. Msafara mkubwa ulikuwa unapita katika mji wa Neishabur hapa Iran, ambapo kwa siku kadhaa wakazi wake walikuwa wamejitayarisha kwa lengo la kumkaribisha Imam. Wakati msafara ulipoingia mjini hapo watu walianza kunong'onezana na hapo machozi ya furaha na upendo yakaanza kuwabubujika. Kila mtu alianza kudhihirisha hisia zake kwa njia tofauti. Makaribisho ya wakazi wa mji huo yalikuwa makubwa kiasi kwamba msafara ulilazimika kusimama. Wote walikuwa na hamu kubwa ya kuona na kumsikia Imam akizungumza, ambapo alitumia fursa hiyo kuwahutubia.
Katika mazingira hayo ya kimya kikubwa, Imam AS aliwanukulia hadithi ambayo Mwenyezi Mungu alimuhutubu Mtume wake SAW kwa kusema: 'Kalima ya la ilaha Illallah ni ngome yangu, na kila mtu anayeingia katika ngome hii, huwa amesalimika kutokana na adhabu yangu.' Baada ya kusoma hadithi hiyo Imam Ridha AS alisema kuwa yeye pia ni sharti la kuingia kwenye ngome hiyo. Alisema: 'Lakini kwa kuzingatia masharti yake na mimi ni moja ya masharti hayo.' Kwa maneno hayo, Imam Ridha AS alibainisha wazi nafasi muhimu ya Ahlul Beit AS ambapo yeye ni mmoja wao, katika kuongoza umma wa Kiislamu.
Sisi pia tunazielekeza nyoyo zetu kwenye ugeni wa haram angavu ya Imam Ridha na kumtumia salama kwa kusema: 'Salamu ziwe juu yako ewe Ali bin Musa ar-Ridha AS ! Salamu ziwe juu yako ewe mjukuu mtakatifu wa Mtume wa Mwenyezi Mungu! Salamu za dhati za waumini wote wa dunia ziwe juu ya uwepo wako ewe chemchemi ya maarifa na hekima!

Imam Ridha (as) alizaliwa mwaka 148 Hijiria sawa na 765 Miladia katika mji matakatifu wa Madina. Baada ya kupata mafunzo na kulelewa na baba yake mtukufu Imam Musa Kadhim AS Imam alikuwa tayari kubeba jukumu zito la kuuongoza umma wa Kiislamu. Alikuwa chemchemi ya elimu na fadhila. Aliridhia uamuzi wa Mwenyezi Mungu katika kila kitendo na neno alilosema. Ni kutokana na sifa hiyo ndipo akaitwa kwa lakabu ya Ridha, yaani mtu anayeridhia kila jambo linalotoka kwa Mwenyezi Mungu. Imam Ridha aliwaongoza Waislamu kwa muda wa miaka 20 ambapo sehemu kubwa ya uongozi huo ulitimia mjini Madina na kumalizia miaka mitatu ya uimamu wake akiwa mjini Marw katika ardhi ya Khorasan. Imam alilazimishwa na Ma'mun, mtawala wa ukoo wa Bani Abbas kuuhama mji wa Madina na kuelekea Marw yaliyokuwa makao makuu ya utawala wao. Katika zama hizo, Marw ulikuwa kituo cha elimu cha Khorasan. Imam pia alitumia fursa hiyo na kuanzisha harakati kubwa ya kielimu. Kutokana na maslahi ya kisiasa, Ma'mun alijaribu kujikurubisha kwa Imam AS lakini wakati huohuo akifanya njama za kudhoofisha shakhsia yake ya kielimu kwa kuandaa mihadhara na mijadala ya kielimu ya wanazuoni. Imam (as) alikuwa akiwashinda wasomi mashuhuri katika mijadala hiyo na kuwaathiri pakubwa kutokana na elimu kubwa na hoja za nguvu na madhubuti alizokuwa akizitumia katika mijadala hiyo.
Uislamu ni dini ambayo inakaribisha maswali tofauti na hakuna hata sehemu moja ambapo Maimamu (as) wamewahi kuulizwa swali na kukataa au kukwepa kulijibu. Imam Ridha AS pia ambaye alibeba jukumu zito la kuuongoza umma wa Kiislamu daima alikuwa akikaribisha maswali kutoka kwa wengine na kuwa tayari kushiriki kwenye mijadala mbalimbali ya kielimu. Mijadala ya kielimu ya Imam Ridha (as) ilikuwa na mchango mkubwa katika kuimarisha na kueneza utamaduni wa Kiislamu. Katika mijadala hiyo Imam (as) alikuwa na lengo la kuwaongoza watu na kamwe hakufikiria juu ya kushindana wala kujiona kuwa mbora zaidi. Alikuwa akitumia mbinu za hoja kuthibitisha ukweli wa itikadi za Kiislamu kwa sababu migongano ya kifikra haiwezi kuondolewa bila kutumiwa hoja za kifikra. Imam AS alikuwa akisema: 'Iwapo watu watajua uzuri na ladha ya maneno yetu Ahlul Bait bila shaka watatufuata.' Ni mazungumzo na mijadala hiyohiyo ya kielimu ndiyo iliyokuwa ikiwabadilisha maadui wa Maimamu kuwa marafiki.

Imam Ridha AS ambaye alikuwa akifahamu vyema mbinu za majadiliano alikuwa akiheshimu na kufuata sheria zote za majadiliano. Uzingatiaji wa viwango vya utamaduni katika zama hizo na kuchaguliwa ibara na maneno yanayofaa kwa kuzingatia uwezo wa kifikra na kielimu wa upande wa pili ni mambo yaliyokuwa yakipewa umuhimu mkubwa na Imam AS katika mijadala yake. Katika mijadala yake na Wakristo alikuwa akizingatia imani na masuala ya pamoja na kutumia hoja zinazokubaliwa na Wakristo hao katika kuthibitisha ukweli wa imani ya Kiislamu.
Licha ya kuwa na kiwango kikubwa cha elimu lakini Imam hakuthubutu kuudunisha wala kudhalilisha upande wa pili katika mijadala yake ya kielimu. Imam alikuwa akiwaheshimu watu wote bila kujali imani, rangi na dini zao. Tunaona katika mjadala wake na mtu mmoja ambaye hakumwamini Mwenyezi Mungu kwa jina la Imran as-Sabi kwamba tabia nzuri na ya kuvutia ya Imam pamoja na hoja zake madhubuti za kuthibitisha mambo zilimpelekea mtu huyo kusilimu na kumwamini Imam AS. Katika kipindi chote cha mjadala wao Imam alikuwa akimwita Sabi kwa jina lake la mwanzo jambo ambalo bila shaka lilikuwa na athari kubwa katika kujenga urafiki na kumuondolea hali ya hofu na woga mbele ya Imam AS. Katika kujibu maswali ya Imrani as-Sabi Imam alikuwa akimuuliza: 'Je, umeelewa ewe Imran?' Tabia hiyo ya kuvutia ya Imam ilimfanya pia Imran amjibu Imam kwa heshima kwa kusema: 'Nam bwana wangu.'

Lengo la mjadala linapasa kuwa ni kufikiwa ukweli na lengo hilo huthibiti pale mjadala unapofanyika mbali na taasubi na uadui usio na msingi. Kutokana na kuwa na maadili ya hali ya juu, Imam hakuwahi kuutuhumu upande wa pili kwa kusema uongo na wala hakuwahi kutaja jambo ambalo lingepelekea upande wa pili kuhisi kuwa unadharauliwa na kudhalilishwa. Daima alikuwa akikosoa kosoro za kiitikadi na kifikra na wala sio shakhsia ya watu aliokuwa akijadiliana nao. Mihadhara na mijadala ya Imam Ridha AS ilikuwa na baraka nyingi kwa ulimwengu wa Kiislamu, kukiwemo kuthibitishwa kwa moyo wa uhuru kwenye Uislamu. Katika mijadala hiyo Imam AS alithibitisha kwamba Uislamu haukuenezwa duniani kwa mabavu na ncha ya upanga kama wanavyodai maadui na waongo, na alitoa mfano wa wazi jinsi kiongozi mkubwa wa Kiislamu anavyowapa wapinzani wake fursa ya kukosoa na kutoa mitazamo yao kuhusu masuala tofauti hata kama itakuwa ni ya kupinga Uislamu na Tauhidi, bila ya kuhofu wala kuogopa lolote. Baraka nyingine za mijadala hiyo ni kuwa Imam Ridha AS aliitumia vyema katika kueneza maarifa ya Kiislamu na kufunga njia za wapinzani na maadui waliotaka kuidhuru dini hii tukufu. Alitumia mihadhara hiyo kufichua njama zilizokuwa zikifanywa na maadui kwa ajili ya kupotosha Uislamu sahihi kwa kunukuu elimu za wageni na kuzisambaza kwenye Uislamu.
Ni matumaini yetu kwamba sote tutafuata mbinu na njia hii ya Mtume AS na Ahlul Bait wake AS katika kumulika njia ya Waislamu katika zama zote. Kwa mara nyingine tena tunatoa mkono wa pongezi na fanaka kwa Waislamu wote duniani na hasa wafuasi wa Ahlul Beit AS kwa mnasaba huu adhimu wa kuadhimishwa uzawa wa Imam Ridha AS.

3522514

captcha