IQNA

Kenya kukabiliana na Madrassah zenye kueneza misimamo mikali ya kidini

0:23 - December 04, 2016
Habari ID: 3470714
IQNA: Serikali ya Kenya imeazimia kukabiliana na Madrassah zenye misimamo mikali ya kidini hasa katika eneo linalopakana na Somalia kaskazini mashariki mwa nchi hiyo.

Kwa mujibu wa mwandishi wa IQNA, serikali ya Kenya imeanzisha kampeni kubwa ya kuwasaka watu wasiokuwa raia wa nchi hiyo ambao wanafanya kazi katika shule za Kiislamu maarufu kama Madrassa au Duksi katika eneo la kaskazini mashariki.

Akizungumza hivi karibuni (Novemba 17) katika mkutano na maimamu wa kaunti ya Garissa katika kikao kuhusu kuleta amani na kutatua migogoro, Bw. Mahmoud Saleh mratibu wa serikali katika eneo kaskazini mashariki alisema idadi kubwa ya madrassah zimewaajiri kinyume cha sheria waalimu kutoka Ethiopia na Somalia. Alisema baAdhi ya walimu hao wana malengo machafu ya kueneza misimamo mikali ya kidini na hivyo serikali itachukua hatua kukabiliana na hali hiyo kutokana na tishio kubwa la kigaidi nchini humo.

"Tunahitaji kufahamu ni vipi waliingia Kenya na ni nani anayewafadhili. Hatuna tatizo na wageni kuja katika nchi yetu lakini wanapaswa kufuata taratibu," alisema Saleh.

Aidha afisa huyo wa serikali ya Kenya amewataka maimamu na wahubiri wengine wa Kiislamu kushirikiana na taasisi za usalama kwani wanaheshimiwa na wananachi na wanaweza kuwa na mchango mkubwa katika kukabiliana na tatizo la ugaidi katika eneo hilo.

3550456

captcha