IQNA

Iran yamlaani Trump kwa kuwazuia Waislamu kuingia Marekani

19:54 - January 29, 2017
Habari ID: 3470821
Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imelaani vikali uamuzi wa serikali ya Marekani kuzuia Waislamu kuingia nchini humo ikisema kuwa, huko ni kuuvunjia heshima waziwazi ulimwengu wa Kiislamu na taifa la Iran.

Kwa mujibu wa mwandishi wa IQNA, Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran ilitoa taarifa hiyo Jumamosi na kusema kuwa, Uamuzi wa serikali ya Marekani wa kuwazuia Waislamu kuingia nchini humo, licha ya kudaiwa kuwa umechukuliwa kwa lengo la kukabiliana na ugaidi na kulinda usalama wa wananchi wa Marekani, lakini kwa hakika ni zawadi kwa makundi yenye misimamo mikali katika eneo la Mashariki ya Kati.

Katika taarifa yake hiyo, Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran imesema: Wakati jamii ya kimataifa ikiwa inahitajia mazungumzo na kuchukuliwa hatua za kimsingi za kukabiliana na misimamo mikali na katika hali ambayo Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa limekubaliana na pendekezo la Iran la kushiriki mataifa yote ya dunia katika vita dhidi ya ugaidi na machafuko, serikali ya Marekani imeamua kuchukua hatua zisizo za kimantiki na kufanya ubaguzi wa wazi dhidi ya raia wa nchi za Kiislamu, suala ambalo bila ya shaka litatumiwa vibaya na makundi yenye misimamo mikali kueneza machafuko duniani.

Taarifa ya Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran imeongeza kuwa, uamuzi huo wa Marekani unawalenga moja kwa moja wananchi wa Iran na kitendo hicho ni kulivunjia heshima taifa hili na wakati huo huo ni kudhihirisha dhati ya kiadui ya Marekani dhidi ya wananchi wa Iran, licha ya kwamba huko nyuma viongozi wa Marekani walikuwa wakijifanya kuwa hawana chuki na wananchi wa Iran.

Balozi wa Uswisi kufikishia Marekani malalamiko ya Iran

Wakati huo huo, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imemuita Balozi wa Usiwis mjini Tehran na kumkabidhi malalamiko rasmi kufuatia hatua ya rais wa Marekania kupitisha sheria za kibaguzi za kuwazuia raia wa Iran na nchi zingine sita za Kiislamu kuingia nchini humo.

Katika mkutano huo wa Jumapili, Mkurugenzi wa Masuala ya Amerika katika Wizara ya Mambo ya Nje, Mohammad Keshavarz-Zadeh, amemkabidhi Balozi wa Uswisi mjini Tehran, Giulio Haas, barua rasmi ya malalamiko dhidi ya Marekani. Ubalozi wa Uswisi mjini Tehran ndio unaowakilisha maslahi ya Marekani nchini Iran.

Mwanadiplomasia huyo wa Uswisi amefahamishwa kuwa hatua ya rais Donald Trump wa Marekani kuwapiga marufuku Waislamu kuingia nchini humo ni ya kibaguzi, haikubaliki na inakiuka mikataba ya kimataifa ya haki za binadamu pamoja na mapatano yaliyotiwa saini kuhusu masuala ya visabaina ya Tehran na Washington Agosti mwaka 1955.

Keshavarz-Zadeh amemfahamisha balozi wa Uswisi kuwa, kuna umuhimu wa kulindwa haki za raia Wairani na kuongeza kuwa, Wairani wamekuwa waathirika wa makundi ya kigaidi yanayopata himaya ya Marekani kwa miongo kadhaa sasa. Aidha amesema Wairani hawajawahi kuhusika na oparesheni yoyote ya makundi ya kigaidi.

Balozi wa Uswisi mjini Tehran amesema ana habari kuhusu amri hiyo ya Trump kuhusu Iran na kuongeza kuwa atawasilisha malalamiko ya Iran kwa Wizara ya Mambo ya Nje ya Marekani.Iran yamlaani Trump kwa kuwazuia Waislamu kuingia Marekani

Itakumbukwa kuwa, Rais Donald Trump wa Marekani Ijumaa alitia saini amri ya kuwazuia Waislamu kuingia nchini humo ambapo hivi sasa kutakuwa na vizingiti kwa wahamiaji na wakimbizi kwa lengo la kuwazuia watu aliowataja kuwa, 'magaidi wa Kiislamu wenye misimamo mikali' kuingia katika nchi hiyo. Nchi za Kiislamu ambazo raia wake wamepigwa kuingia Marekani kwa muda wa siku 90 ni pamoja na Libya, Sudan, Somalia, Yemen, Iraq, Syria na Jamhuri ya Kiislamu ya Iran. Hatua hiyo ya Trump imeibua hasira na maandamano Marekani na kote duniani.

3568127/3567386
captcha