Muhammad Ali Junior, mmoja wa watoto wa marehemu Muhammad Ali, alitiwa
mbaroni katika uwanja wa ndege wa jimbo la Florida wakati alipokuwa
akirejea kutoka nchini Jamaica kuingia Marekani. Habari zaidi zinasema
kuwa, baada ya kutiwa mbaroni mwana huyo wa Muhammad Ali alihojiwa kwa
masaa mawili.
Muhammad Ali Junior alizaliwa katika mji wa Philadelphia katika jimbo
la Pennsylvania nchini Marekani huku akiwa na pasi ya kusafiria ya nchi
hiyo. Junior anaishi nchini Jamaica pamoja na mama yake, Khalilah
Camacho Ali. Wakili wa mwana huyo wa Muhammad Ali, kwa jina la Chris
Manshny amesema kuwa kijana huyo wa mwanamasumbwi mashuhuri duniani na
mama yake walitiwa mbaroni katika uwanja huo wa ndege wa Florida mwezi
huu kutokana na kuwa na majina ya Kiarabu.
Kwa mujibu wa wakili huyo, Bi, Khalilah Camacho Ali na mwanaye
waliachiliwa, mara baada ya kuonyesha picha inayomuonyesha yeye akiwa na
marehemu mume wake huku wakiwa tayari wamehojiwa kwa muda usiopungua
masaa mawili.
Tangu Rais Donald Trump wa Marekani aliposaini marufuku ya
kuzuiwa raia wa nchi saba za Kiislamu kuingia nchini humo, Waislamu
wamekuwa wakikumbwa na madhila mbalimbali ndani ya taifa hilo
linalojinadi kuwa mtetezi wa haki za binaadamu duniani. Hii ni katika
hali ambayo mahakama kadhaa za nchi hiyo zimetaka kutupiliwa mbali
marufuku hiyo ya Rais Trump.
Uchunguzi wa maoni unaonyesha kuwa, asilimia 60 ya Waislamu wa Marekani
wanashtakia na kulalamikia ubaguzi, taasubi dhidi ya Uislamu pamoja na
propaganda na hisia za chuki dhidi ya dini ya Kiislamu. Vyombo vya
habari vya Marekani navyo vimekuwa vikieneza propaganda na hisia za
chuki dhidi ya Uislamu na Waislamu na kufanya njama za kuonyesha kuwa
dini hiyo tukufu haina tofauti na misimamo ya kuchupa mipaka. Trump
ambaye katika kampeni zake za uchaguzi alionesha wazi misimamo yake ya
chuki dhidi ya Uislamu na Waislamu, anaonekana kushikilia misimamo yake
hiyo hadi sasa ikiwa ni majuma kadhaa tu kabla ya kuapishwa na kuanza
rasmi kipindi chake cha uongozi.