IQNA

Jeshi la Iraq lamuangamiza kinara nambari mbili wa ISIS huko al-Anbar

10:40 - April 02, 2017
Habari ID: 3470915
TEHRAN (IQNA)Jeshi la Iraq limetangaza kumuua kinara nambari mbili wa kundi la magaidi wakufurishaji wa ISIS au Daesh katika shambulizi la anga, magharibi mwa mkoa wa al-Anbar nchini humo.

Kwa mujibu wa habari iliyotolewa na Shirika la Habari la Alsumaria News, ndege za jeshi la Iraq zimeshambulia ngome ya kijeshi ya kundi hilo la ISIS eneo la magharibi mwa al-Anbar na kusababisha kuuawa kiongozi huyo wa pili baada ya Abubakar al-Baghdadi kwa jina la Ayad Hamid KhalafAl-Jumaili, maarufu kwa jina la Abu Yahya.

Al-Jumaili anatambuliwa kwa cheo cha waziri wa vita wa kundi hilo la ukufurishaji la ISIS, Jeshi la Iraq limeongeza kuwa, shambulizi hilo limepelekea pia kuuawa magaidi wengine wawili wa ngazi ya juu wa genge hilo wa kwanza akiwa ni Turki Jamal al-Dailami, maarufu kwa jina la Abu Hajar, kiongozi wa masuala ya kijeshi wa genge hilo na wa pili akiwa ni Salim Mudhafar al-Ajmi, maarufu kwa jina la Abu Khitwab, mkuu wa ofisi za ISIS. Habari zinaeleza kuwa, mkoa wa al-Anbar unashuhudia mashambulizi ya anga ya jeshi la Iraq yanayotekelezwa kwa lengo la kudhibiti maeneo mengine yaliyosalia ambayo yalikuwa chini ya udhibiti wa kundi hilo.

Hivi karibuni Waziri Mkuu wa Iraq, Haider al-Abadi alisema kuwa ushindi dhidi ya kundi la kigaidi na ukufurishaji la ISIS unakaribia.

Huku akiashiria ushindi wa jeshi la Iraq kwa kushirikiana na harakati ya wananchi ya Hashdu Ash-Sha'abi, alisema kuwa, jeshi la nchi yake limekaribia sana kulishinda genge la kigaidi la ISIS. Waziri Mkuu wa Iraq alisisitizia umuhimu wa wananchi na jamii ya kimataifa kuendelea kuiunga mkono Iraq katika mapambano yake dhidi ya ugaidi.

3586265

captcha