IQNA

Shehbaz Sharif awasilisha pendekezo la kuwa waziri mkuu Pakistan baada ya Imran Khan kuuzuliwa

23:33 - April 10, 2022
Habari ID: 3475108
TEHRAN (IQNA)- Mwanasiasa wa upinzani Shehbaz Sharif amewasilisha pendekezo la kutaka kuteuliwa kuwa waziri mkuu wa Pakistan baada ya Imran Khan kuuzuliwa na bunge.

Kura ya kutokuwa na imani na Imran Khan imepigwa jana Jumamosi jioni baada ya masaa kadhaa ya mvutano ambao ulipelekea spika wa bunge kujiuzulu. Serikali ya muda inatazamiwa kuongoza nchi kaba ya uchaguzi mkuu kufanyika.

Wabunge wa upinzani waliweza kupata kura 174 katika bunge lenye wabunge 342 na hivyo kufanikiwa kupata kura za kutosha za kumuondoa madarakani Imran Khan. Bunge sasa linatazamiwa kukutana Jumatatu kumchagua waziri mkuu mpya ambapo kinara wa upinzani Shehbaz Sharif anasema ana matumaini makubwa kuwa atachaguliwa kuwa waziri mkuu katika nchi hiyo yenye idadi ya watu milioni 220.

Katika kikao cha jana bungeni, kwa mara ya kwanza katika historia ya Pakistan kulisikika nara za 'Mauti kwa Marekani' ambazo zilikuwa zikitolewa na wabunge wanaomuunga mkono Imran Khan.

Wiki iliyopita, Imran Khan aliituhumu serikali ya Marekani kuwa imechochea wabunge kumuondoa madarakani. Alifichua kuwa afisa mwandamizi wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Marekani anayeshughulikia Kusini mwa Asia Donald Lu alimtahadharisha balozi wa Pakistan Marekani, Asad Majeed kuwa, kutakuwa na matokeo mabaya iwapo kura hiyo ya kutokuwa na imani na waziri mkuu haitafanikiwa.

Imran Khan amesisitiza kuwa Marekani imehusika kikamilifu katika njama ya kuipindua serikali yake kwa kushirikiana na baadhi ya wabunge wahaini.

Katika miezi ya hivi karibuni Imran Khan amekuwa akichukua misimamo huru ya sera za kigeni ikiwa ni pamoja na kuwa na uhusiano wa karibu na Russia pamoja na China jambo ambalo limeikera sana Marekani. Aidha amekuwa mstari wa mbele kukosoa sera za chuki dhidi ya Uislamu katika nchi za Magharibi.

3478435

captcha