IQNA

Mashindano ya Qur'ani

Qari wa Iran ashika nafasi ya tatu katika Mashindano ya Kimataifa ya Qur'ani Tanzania

18:44 - March 25, 2024
Habari ID: 3478574
IQNA - Mwakilishi wa Iran katika Mashindano ya 20 ya Kimataifa ya Qur'ani ya Tanzania ameshika nafasi ya tatu.

Sherehe ya kufunga mashindano ambapo washindi walitangazwa na kutunukiwa, katika hafla iliyofanyika mwishoni mwa wiki.

Kulingana na jopo la majaji, Ilyas al-Mahyawi kutoka Morocco alipata nafasi ya kwanza na mshindi wa pili alikuwa Shihab Ahmed kutoka Misri.

Tuzo la nafasi ya tatu lilikwenda kwa qari wa Iran, Ustadh Mohsen Qassemi.

Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Mwalimu Julius Nyerere ndicho kilichokuwa mwenyeji wa hafla hii ya kimataifa ya Qur'ani ambayo imefanyika katika mwezi mtukufu wa Ramadhani.

Washiriki wengine walikuwa kutoka nchi kadhaa ikiwemo nchi mwenyeji pamoja na Misri, Uturuki, Afrika Kusini, Morocco, Palestina, Kenya, Bangladesh, Vietnam, Greenland, Iran, Msumbiji, na Visiwa vya Comoro.

Jopo la majaji hao lilijumuisha wataalamu wa Qur’ani wanaojulikana kimataifa kama vile Sheikh Othman al-Hiwari na Sheikh Ali al-Shamisi kutoka Misri, Sheikh Muti al-Rahman al-Miskari kutoka Morocco, Sheikh Abdul Wahab al-Sirari kutoka Yemen, Sayid Salih al- Ahdal kutoka Kenya, Sheikh Ismail Lunt kutoka Afrika Kusini, na Sheikh Abullah al-Munzari na Abdul Mannan Muhammad kutoka Tanzania.

Mgeni maalum katika hafla hiyo ya kuhitimisha mashindano hayo ya Qur’ani Tukufu alikuwa Dakta Hussein Mwinyi, rais wa Zanzibar, ambaye aliangazia Hadithi kutoka kwa Mtukufu Mtume Muhammad (SAW) kuhusu Qur’ani Tukufu: “Walio bora miongoni mwenu (Waislamu) ni wale wanaojifunza Qur’ani na kuifundisha.”

Ameyataja mashindano ya Qur'ani kuwa ni programu bora zaidi kwa Waislamu na pia akasisitiza umuhimu wa juhudi za kuimarisha umoja wa Kiislamu.

Mashindano hayo ni miongoni mwa matukio maarufu ya Qur'ani Afrika Mashariki, yanayoandaliwa kila mwaka na Taasisi ya Khidmatul Quran.

Ni taasisi ya Kiislamu ambayo inayofanya kazi ya kukuza utamaduni na mafundisho ya Qurani nchini Tanzania.

Mbali na kuandaa mashindano ya Qur'ani, taasisi hiyo hualika pia maqarii wa kimataifa  kuja Tanzania kuhudhuria programu za Qur'ani nchini humo.

 

4206973

 

Habari zinazohusiana
captcha