IQNA

Uganda kuchunguza mauaji ya Waislamu mwaka 1979

16:30 - January 18, 2016
Habari ID: 3470056
Serikali ya Uganda imeanzisha uchunguzi kuhusu mauaji ya Waislamu 67 nchini humo mwaka 1979 baada ya kupinduliwa mtawala wa wakati huo Idi Amin.
Akitangaza kuanza uchunguzi huo, Waziri Mkuu Ruhakana Rugunda amesema kumeundwa jopo maalumu ‘kufanya uchunguzi kamili wa kubainisha ukweli kuhusu taarifa za kuuawa kwa Waislamu mwaka 1979 na jopo hilo linapaswa kumpa ripoti katika kipindi cha wiki tatu. Imearifiwa kuwa uchunguzi huo utaongozwa na wakili mkuu wa serikali nchini Uganda.

Katika ghasia zilizozuka baada ya kuangushwa Amin Aprili mwaka 1979, watu waliokuwa na silaha walivamia vijiji viwili vya wilaya ya Sheema kusini magharibi mwa Uganda na kuwaua Waislamu 67 na kisha kuitupa miili yao ndani ya Mto Rwizi.

Misikiti tisa na makumi ya nyuma za Waislamu ziliteketezwa mbali na kuharibiwa mashamba ya Waislamu. Wengi walilazimika kukabidhi ardhi zao ili kuokoa maisha yao.

Waislamu hao walishambuliwa kwa kushukiwa kuwa walikuwa wanamuunga mkono Amin ambaye inadaiwa kuwa wakati wa kipindi cha miaka minane ya utawala wake idadi kubwa ya watu waliuawa kiholela.

Rugunda ametoa tangazo hilo Jumamosi hii kufuatia amri ya Rais Yoweri Museveni ambaye ametaka kulipwa fidia familia za waliouawa au mali zao kuporwa katika tukio hilo.

Msemaji wa Baraza Kuu la Waislamu Uganda Hajji Nsereko Mutumba ameelezea matumaini yake kuwa amri ya Museveni itatekelezwa.

Umar Kassaja Mutono mwanachama ya manusura wa mauaji ya Sheema amesema Waislamu waliuawa kinyama wakati wa hujuma hiyo ya kikatili.


3468214
captcha