IQNA

Gambia yasema itaheshimu haki za wote katika mfumo wake wa Kiislamu

23:15 - March 22, 2016
Habari ID: 3470210
Serikali ya Jamhuri ya Kiislamu ya Gambia imesema itaheshimu haki za raia na wakaazi wote nchini humo wakiwemo Wakristo na wengine.

Katika taarifa, waziri wa habari wa Gambia Sheriff Bojang amekosoa baadhi ya mitandao ya intaneti nchini humo na vyombo vya habari vya kigeni kwa kueneza propaganda dhidi ya serikali ya Jamhuri ya Kiislamu iliyotangazwa nchini humo.

Mwezi Desemba mwaka jana Rais Yahya Jammeh wa Gambia aliitangaza nchi hiyo ya Kiafrika kuwa Jamhuri ya Kiislamu.

Akitangaza hatua hiyo, Rais Jammeh alisema kuwa, kuanzia sasa mfumo wa Jamhuri ya Kiislamu unatawala nchini humo ikiwa ni katika juhudi za kutoa utambulisho kwa thamani za kidini.

Rais Yahya Jammeh alisema kuwa, kwa kuwa raia waliowengi wa nchi hiyo ni Waislamu, Gambia haiwezi kuendelea kuvumilia turathi za kikoloni.

Rais wa Gambia alisisitiza kuwa, wafuasi wa dini nyingine nchini humo hawatabughudhiwa na wanaweza kuishi kulingana na mafundisho ya dini zao.

Rais Jammeh ambaye mwaka 2013 alitangaza kujitoa nchi hiyo katika Jumuiya ya Madola, Commonwealth na kuitaja kuwa ni ukoloni mamboleo, anataraji nchi za Kiarabu zitaisaidia nchi yake ili iweze kuziba pengo la misaada iliyokatwa na itakayokatwa ya madola ya Magharibi. Machi mwaka huu serikali ya Gambia ilibadilisha lugha yake rasmi ya Kiingereza na kuifanya kuwa Kiarabu.

Gambia ina wakazi milioni moja na laki nane huku asilimia 95 wakiwa ni Waislamu. Gambia ilikoloniwa na Uingereza hadi mwaka 1965 ilipopata uhuru.

Nchi hiyo inategemea zaidi kilimo na utalii kama sekta kuu na uti wa mgongo wa uchumi wake.

3459377

captcha