IQNA

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu

Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imesimama imara na kwa nia isiyotetereka katika kukakbiliana na adui

20:16 - September 11, 2023
Habari ID: 3477583
TEHRAN (IQNA)- Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu leo Jumatatu ameonana na wananchi wa mikoa miwili ya "Sistan na Baluchistan" na ule wa "Khorasan Kusini" na kusisitiza kwamba, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imesimama imara na kwa nia isiyotetereka katika kukakbiliana na adui.

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu aidha amesema: Kuvuruga umoja wa kitaifa na kudhoofisha usalama wa taifa hili, ni malengo makuu ya maadui wa Iran lakini na sisi tumesimama imara na hatutetereki katika kukabiliana na adui. Tuna yakini kwamba maadui wa Iran yetu azizi hawawezi kufanya upuuzi wowote iwapo wananchi na viongozi wao wataendelea kuwa macho na kutoghafilika.

Ayatullah Sayyid Ali Khamenei ameongeza kuwa, dunia ya leo iko ukingoni mwa mabadiliko makubwa ambayo sifa yake kubwa ni kudhoofika madola makubwa ya kikoloni na kudhihiri madola makubwa mapya ya kieneo na kimataifa. 

Kiongozi Muadhamu ametoa ushahidi kwenye matamshi ya baadhi ya duru za nchi za Magharibi na kusema kuwa, vielelezo vya nguvu za Marekani kama katika upande wa masuala ya kiuchumi, vinaendelea kushuka na kuongeza kuwa, hata nguvu za Marekani za kupindua tawala za mataifa mengine duniani zinaonekana waziwazi jinsi zinavyoporomoka.

Amesema, kushindwa Marekani huko nchini Syria na kulazimika dola hilo kukimbia kwa madhila nchini Afghanistan, ni mifano miwili ya wazi ya kuporomoka nguvu za Marekani. Amesisitiza kuwa, madola mengine ya kiistikbari nayo yamekumbwa na hali hiyo na tumeaona katika siku za hivi karibuni jinsi mwamko wa kuipinga Ufaransa ulivyoingia kasi barani Afrika huku wananchi wa nchi hizo za Afrika wakiunga mkono kwa wingi harakati zilizo dhidi ya Ufaransa katika nchi zao.

Ayatullah Khamenei vilevile amesema, njama za Marekani haziishii tu kwa Iran na kusisitiza kuwa, Marekani leo hii inaendesha njama dhidi ya nchi za Iraq, Syria, Lebanon, Yemen, Afghanistan na hata dhidi ya nchi za Ghuba ya Uajemi ambazo ni marafiki zake wa jadi.

4168157

Habari zinazohusiana
captcha