Ayatullah Udhma Sayyid Ali Khamenei, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya
Kiislamu aliyasema hayo Jumatano jioni mjini Tehran, aliponana na Rais wa
Jamhuri ya Kiislamu na wajumbe wa Baraza la Mawaziri la Iran ikiwa ni katika
kuendeleza mialiko yake ya Ramadhani na futari kwa watu wa kada na daraja mbali
mbali nchini. Kiongozi Muadhamu ametumia fursa hiyo kubainisha hekima kadhaa
zilizomo kwenye kitabu cha Nahjul Balagha.
Ameashiria matamshi ya Amirul Muminin, Imam Ali (Alayhis Salaam) kuhusiana na
namna watu wanavyopasa kufanya wakati inapotokea fitna na kusema: Imam Ali
(Alayhis Salaam) anatuusia kwamba, wakati inapotokea fitina na ikawa ni jambo
zito kutofautisha baina ya haki na batili, tuchukue hatua ambazo hazitaisaidia
fitna kwa hali yoyote ile.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ameongeza kuwa: Wakati inapotokezea
fitna kama ile iliyotokea nchini Iran mwaka 2009, si sahihi kuruhusu masuala
kama matamshi, kunyamaza kimya, uchukuaji hatua bali hata namna ya uangaliaji
na utazamaji wa mambo, yasaidie kupata nguvu fitna.
Ayatullah Udhma Khamenei ameongeza kuwa: Tab'an inawezekana wakatokezea watu
wakawa hawako tayari kujitokeza hadharani kukabiliana na fitna kutokana na
mitazamo yao maalumu, lakini si sahihi kumtumia vibaya mtu huyo kwa ajili ya
kukuza fitna hiyo.
Vile vile amegusia hekima nyingine ya Imam Ali (Alayhis Salaam) ndani ya Nahjul
Balagha kwa kuzungumzia suala la kuangalia cheo kwa tamaa na kukiona kuwa ni
fursa ya kujitajirisha na kupata upendeleo maalumu na kusema: Cheo ni dhamana,
hivyo kuwa na mtazamo wa tamaa namna hiyo kuhusu cheo, hupelekea mtu kupoteza
heshima yake na kudhalilika.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ametoa ufafanuzi zaidi kuhusiana na
suala hilo kwa kugusia suala la baadhi ya watu waliotumia vyeo vyao kutwaa
kiasi kikubwa cha mishahara na kusisitiza kwamba: Suala la mishahara mikubwa
kupindukia kwa hakika ni kuhujumu matukufu ya nchi lakini kila mtu anapaswa
kutambua kuwa, jambo hilo ni katika masuala ya nadra kutokea na kwamba sehemu
kubwa ya wakuu na viongozi wa taasisi mbali mbali nchini ni watu wasafi. Hata
hivyo, pamoja na kwamba watu waliofanya hivyo ni wachache lakini kitendo chao
hicho ni kiovu na ni kibaya sana na lazima sheria ifuate mkondo wake
kukabiliana nao.
Vile vile amegusia amri iliyotolewa na mheshimiwa Rais kwa Makamu wa Kwanza wa
Rais ya kulifuatilia vilivyo suala hilo na kusema: Ufuatiliaji wa jambo hilo
haupaswi kuchelewa, bali inabidi hatua kali zichukuliwe haraka na wananchi
waelezwe matokeo yake.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ameongeza kuwa: Kwa mujibu wa
taarifa zilizonifikia, kiwango cha mishahara ya wakuu katika taasisi mbali
mbali nchini ni cha kawaida na kinakubalika na kwamba wakuu wanaopokea
mishahara mikubwa kupindukia ni wachache. Pamoja na hayo, hatua kali sana
zinapaswa kuchukuliwa hata kama wakuu hao wanaochukua mishahara ya namna hiyo
ni wachache sana.
Katika sehemu ya mwisho ya matamshi yake, Ayatullah Udhma Khamenei ameashiria
hekima nyingine za Imam Ali (Alayhis Salaam) zilizomo ndani ya kitabu cha
Nahjul Balagha na kusema: Inabidi kuchunga ndimi zetu wakati wote, kwani sehemu
kubwa ya matatizo yanayomkumba mwanadamu huwa yanatokana na ulimi wake.
Amesisitiza kuwa: Matatizo yanayotokana na kutochunga ulimi wakati wa
kuzungumza, baadhi ya wakati huwa yanaishia tu katika kupata madhara mtu
mwenyewe aliyeshindwa kuchunga ulimi wake, lakini baadhi ya wakati jambo hilo
huzusha matatizo katika jamii nzima, hivyo tunapaswa kuchukua tahadhari kubwa
kuhusu suala hilo.
Kabla ya hotuba ya Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu, Hujjatul Islam
Walmuslimin Hassan Rouhani, Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ametoa ripoti
fupi kuhusiana na hatua mbali mbali zilizochukuliwa na serikali yake na mipango
na mikakati yake ya baadaye.
Mwishoni mwa mkutano huo, hadhirina wamesalishwa sala za Magharibi na Isha na
Ayatullah Udhma Khamenei, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu na baadaye
wamekula futari pamoja naye.