IQNA

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu

Muungano wa Magharibi hauna nia ya kweli ya kuangamiza ugaidi

20:43 - October 25, 2016
Habari ID: 3470635
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema nchi zenye misimamo huru zinapaswa kuimarisha uhusiano baina yao na kutoathiriwa na siasa za madola ya kibeberu na Kiistikbari ili kuweza kuzima moto wa hitilafu na mapigano uliowashwa na madola hayo.

Ayatullah Sayyid Ali Khamenei ameyasema hayo leo katika mazungumzo na Bakir Izetbegovic, Mwenyekiti wa Baraza la Urais wa Bosnia Herzegovina aliyeko safarini hapa nchini.

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ameashiria wimbi la ukufurishaji na ugaidi ambalo hivi sasa limesambaa hadi barani Ulaya na kuwepo uwezekano wa hali kuwa mbaya zaidi katika siku za usoni na kuongeza kuwa: "Kidhahiri chimbuko la janga hili ni eneo la Kiarabu, lakini ukweli ni kwamba serikali ya Marekani na baadhi ya serikali za nchi za Ulaya ndio wahusika wakuu wa kuzuka matukio haya".

Ayatullah Khamenei amebainisha kuwa muungano wa kijeshi wa madola ya Magharibi dhidi ya ugaidi si muungano wa kweli na kufafanua kwa kusema: "Hata kama yumkini katika baadhi ya hali muungano huu unaweza kuingia vitani kupambana na magaidi lakini hauna nia ya kweli ya kuung'oa na kuutokomeza ugaidi; si Iraq wala si Syria; na siasa zao mbaya na ovu zitawazidishia matatizo wanadamu siku baada ya siku". Ayatullah Khamenei amesema dawa na tiba ya hali hiyo inapatikana katika kuelewa na kutambua sababu za kujitokeza matatizo hayo na kuwepo irada na nia ya kweli ya kuyatatua; na katika kuashiria moja ya sababu za kujitokeza ugaidi akabainisha kuwa: "Kudhalilishwa vijana Waislamu katika baadhi ya nchi tajiri na zenye nguvu za Ulaya, kunachangia kuwafanya vijana hao kujiunga na makundi potofu ya kigaidi kama ISIS au Daesh; na wakati vijana hawa waliodunishwa wanaporudi Ulaya wanafanya mauaji na uripuaji mabomu".

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ameashiria pia historia ya uhusiano wa kirafiki baina ya Iran na Bosnia Herzegovina na kipindi kigumu na cha machungu cha wakati wa vita vya kulazimishwa dhidi ya wananchi wa nchi hiyo na kueleza kwamba: "Utulivu na amani ni mambo ya lazima ili kuwezesha nguzo zote za uhai wa taifa kuchanua na kustawi".

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Baraza la Urais wa Bosnia Herzegovina amesema amefurahishwa na safari yake mjini Tehran na akayatathmini mazungumzo aliyofanya na viongozi wa Iran kuwa ya mafanikio. Bakir Izetbegovic ameongeza kuwa ana matumaini uhusiano wa kirafiki baina ya nchi mbili utabadilika kuwa ushirikiano athirifu wa kiuchumi kwa manufaa ya pande mbili.

3540812

captcha