IQNA

Iran mwenyeji wa mkutano wa kutetea ukombozi wa Palestina

18:37 - February 19, 2017
Habari ID: 3470856
IQNA: Mkutano wa Kimataifa wa Kuunga Mkono Intifadha ya Palestina utafanyika tarehe 21 na 22 Februari katika mji mkuu wa Iran, Tehran.

Msemaji wa mkutano huo Kadhim Jalali   amesema wageni 700 kutoka nchi 80 duniani watashiriki katika kongamano hilo ambalo litafunguliwa kwa ujumbe wa Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu.

Amesema nara na kaulimbiu kuu ya mkutano huo ni, "Wote kwa Pamoja katika Kuunga Mkono Palestina" na utawaleta pamoja maspika wa mabunge, wabunge, waku wa tume za sera za kigeni katika mabunge, wasomi na wanasiasa wa ngazi za juu, wanaharakati wa kupigania ukombozi Palestina na mashirika yasiyo ya kiserikali yenye kutetea Palestina kote duniani.

Aidha amekumbusha Bunge la Iran, Majlisi ya Ushauri ya Kiislamu , imeandaa makongamano matano ya kuunga mkono Palestina tokea mwaka 1990 wakati bunge hilo lilipopitisha sheria ya kuunga mkono mwamko wa Kiislamu Palestina.

Huku akiashiria njama za Wazayuni kuharibu nembo za Kiislamu katika ardhi za Palestina zinazokaliwa kwa mabavu, hasa Msikiti wa Al Aqsa mjini Quds Tukufu, amesema kuendelea ujenzi wa vitongoji haramu vya walowezi wa Kizayuni, mzingiro wa kinyama katika Ukanda wa Ghaza na kusema kongamano la Tehran linalenga kuhimiza umoja wa Waislamu katika kukabiliana na utawala wa Kizayuni wa Israel.

Duru mpya ya mapambano ya wananchi wa Palestina ambayo ilianza Oktoba 2015 imepewa jila la Intifadha Mpya ya Quds au Intifadha ya Tatu ni tukio muhimu sana katika historia ya mapambano ya ukombozi ya Wapalestina dhidi ya maghasibu. 

Intifahda hiyo ilianza baada ya utawala haramu wa Israel kuwawekea Waislamu vizingiti vya kuswali katika Msikiti wa Al Aqsa ambao ni sehemu ya tatu kwa utakatifu katika Uislamu na qibla cha kwanza cha Waislamu. Mamia ya Wapalestina wameuawa mikononi mwa askari wa utawala dhalimu wa Israel tokea mwamko huo mpya uanze.


captcha