IQNA

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu
21:10 - December 31, 2018
News ID: 3471792
TEHRAN (IQNA)-Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesisitiza kuwa, Palestina itaendelea kuwa taifa lenye nguvu na kwa uwezo wa Mwenyezi Mungu, katika kipindi kisicho mbali sana taifa hilo litaweza kupata ushindi wa mwisho.

Ayatullah Sayyid Ali Khamenei amesema hayo leo Jumatatu mjini Tehran wakati alipoonana na Ziad al-Nakhala, Katibu Mkuu wa harakati ya Jihadul Islami wa Palestina na ujumbe alioandamana nao uliopo hapa Iran kwa ziara rasmi. Kiongozi Muadhamu pia amegusia kipimo kilicho wazi katika kadhia ya Palestina akisema, kwa mujibu wa kipimo hicho, kama watu watashikamana na muqawama watashinda na wakiacha kushikamana na muqawama watashindwa. Amesema, Alhamdulillah kwa uwezo wa Mwenyezi Mungu, hadi hivi sasa wananchi wa Palestina wameshikamana vilivyo na muqawama katika kupambana na utawala wa Kizayuni na ndio maana wamekuwa wakipata ushindi.

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ameongeza kuwa, ushindi mkuu wa wananchi wa Palestina na makundi ya muqawama ni kwamba utawala wa Kizayuni ambao majeshi ya nchi za Kiarabu yameshindwa kukabiliana nao, umepata kipigo kutoka kwa wananchi na wanamuqawama wa Palestina na kwa uwezo wa Mwenyezi Mungu wananchi hao watazidi kupata ushindi katika siku za usoni.

Vile vile amesema, katika vita viwili vilivyopita vilivyoanzishwa na Israel dhidi ya Wapaletina huko Ghaza, utawala wa Kizayuni ulilazimika kuomba kusimamishwa vita baada ya siku 22 na katika vita vilivyofuata baada ya siku nane. Lakini katika vita vya hivi karibuni, utawala wa Kizayuni wa Israel haukuweza kudumu kwenye vita hivyo kwa zaidi ya masaa 48 na hii ina maana ya kuzidi kushindwa na kupigishwa magoti utawala wa Kizayuni wa Israel. Amesema utawala wa Kizayuni utazidi kuporomoka na ushindi wa Wapalestina utaendelea kupatikana madhali bado wameshikamana na muqawama.

Aidha amegusia jinsi kambi ya kibeberu inavyoiwekea mashinikizo makubwa sana Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na kusisitiza kuwa, mashinikizo na vikwazo hivyo kamwe havitaifanya Jamhuri ya Kiislamu iache kutekeleza wajibu wake wa kidini, kibinadamu na kiakili wa kuliunga mkono taifa la Palestina.

3777288

Name:
Email:
* Comment: